Header Ads Widget

WASAMBAA MTANI HUGAWA MALI ZA MAREHEMU (III)

 


Adeladius Makwega-DODOMA


Katika matini yangu iliyotangulia nimeeleza utani katika mazingira mengine yasiyo ya msibani huku kukiwa na utani ambao unaweza sababisha hasara kubwa kwa mtu mwingine.


Kutokana na kuwepo na utani huo hata lugha ya Kisambaa imeubeba utani huo katika lugha yake. Leo hii nautazama utani huo katika lugha ya Kisambaa ulivyo katika misemo, nahau na methali.


 Kwa mfano;


“Kufa kufaana.”


Hapo ikimaanisha kuwa mtu anapofariki ni manufaa kwa mwingine.


“Kimweri ni mdogo, Mungu mkuu.”


Hapo akimaanisha kuwa Kimweri anauwezo mdogo bali Mungu anauwezo mkubwa.


“Shida in kanuni kia hantu kaantoo.”


Kila shida inayokufika itazame kama umakini.


“Shwagho ne ni utumba.”


Hata marehemu/ hata mtu mzee nayeye alikuwa kijana.


Pia utani wa WAKINASEUTA na WAKINAKITUI unaweza kuonekana katika methali hizi:


“Nne udaaha kama isho Tiyo.”


Tiyo ni mzee nani anaweza kumuuliza anaoa lini.


Majibu ya Tiyo yalikuwa kama ifuatavyo


“Nighuukisi name nikeebuntia?”


Kwanini nikimbilie kuoa wakati mimi bado kijana?


Maana yake ni kuwa huyo anayeambiwa kwanza ni kijana siyo mzee anafananishwa na mjomba wake Tiyo ambaye hataki kuoa. Hapo inasisitizwa umuhimu wa kuoa.


“Hana heshima na wavyoengwa iwe ndie umghue wako ama uyokwe.”


Hapo inamaanisha kuwa mtu akiwa na tabia mbaya basi atamuoa bibi yake.


Akimaanisha kuwa ni vizuri jamii kuwa na watu wenye tabia nzuri kwani watapendwa na jamii husika.


A.J. Mshihiri anasimulia kuwa kuna wakati alikwenda kumtembelea babu yake huko Mgwashi na siku hiyo babu yake alikuwa shambani akilima. Babu huyo alikuwa na shamba la miwa kubwa.


Kwa kuwa muda huo alioenda ulikuwa na jua kali A.J Mshihiri anadai kuwa babu yake alikuwa amepumzika. Safari hiyo A. J Mshihiri aliambatana na rafiki zake wawili


Walipofika hapo babu wa Mshihiri aliwaruhusu wajukuu zake kukata miwa ili wale wakiwa hapo shambani na mara walipoambiwa walifanya hivyo. Miwa hiyo walikula kwa muda kidogo alafu wakarudi tena kukata tena miwa mingine.


Walipoanza kukata miwa ya awamu ya pili walimsikia babu yao akisema maneno haya:


“Mashine zia za masingasinga zetatua mbao zabinda miti sana.”


Akimaanisha kuwa mashine za masingasinga zinazopasua mbao zinamalizi miti kweli.


A J Mshihiri anadai kuwa mwanzoni hawakumuelewa babu yao alikuwa akimaanisha nini lakini baadaye walipomuelewa walicheka mno. 


Jambo hilo lilikuwa utani na waliendelea kula miwa na walirejea kukata tena miwa hiyo ya babu yake Mshihiri. Babu huyu hakukaa kimya bali aliendelea kusema maneno mengine.


“Mashine ya sukari Arusha yasaga mighua sana.”


Wakimaanisha kuwa mashine ya kutengeneza sukari ya Arusha inafanya kazi vizuri sana.


“Mwishoni babu yangu alituuliza kama tuna ardhi atusaidie kupanda miwa, huku sisi sote tukibaki na kicheko tu.” Anasema A J Mshihiri.


Funzo alilokuwa akitoa babu huyu ilikuwa kama mtu anapenda kula kitu basi anawajibu wa kupanda mazao hayo , siyo mwingine alime na mwingine aje kula tu na tena  kwa fujo kama vojana hawa walivyokuwa wakila miwa yake.


Kwa hakika mwanakwetu naomba niishie hapo, juu ya utani ndani ya kabila hili la Wasambaa ambao ni wakwe zangu na shemeji zangu. Natambua Balozi Mstaafu Abdi Mshangama, Mzee Yusuph Makamba na wazee wengine wa Kisambaa sijawakwaza kwa mifano kadhaa niliyoitoa, maana nisije kuja Lushoto, Bumbuli na Korogwe mkaniambia kuwa hamnipokei kisa nimeandika vibaya juu ya kabila lenu. Natambua hata nikija huko hamtonilipisha mbuzi wa faini kwani sina kosa nililofanya zaidi ya kueleza kilichomo katika utamaduni wenu tu.


Kukuaga msomaji wa matini zangu nakujulisha kuwa matini ijayo nitawatazama watani wa Wasambaa ambao ni Wapare.


Nakutakia siku njema.


makwadeladius @gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI