Katika sehemu ya kwanza matini haya msomaji wangu utakumbuka kuwa nilikueleza mengi juu ya asili ya Wasambaa kuwa walitokea Kenya, pia nilienda mbali na kutaja aina mbili za Wasambaa wale WAKINASEUTA na WAKINAKITUI.Mwandishi Adeladius Makwega-DODOMA
Pia nilieleza namna WAKINASEUTA walivyotoka Kenya hadi wakafika Handeni, hapo walivyopambana na Wamasai hadi baadhi ya Wasambaa wakakimbilia katika Safu za Milima ya Usambara.
Katika matini hiyo nilidokeza juu ya utani ndani ya kabila hilo unavyofanyika katika misiba. Leo msomaji wangu ninaendelea na utani wa Wasambaa unavyofanyika nje ya misiba.
Mtafiti A. J Mshihiri ambaye alikuwa mzaliwa wa Mgwashi Lushoto Tanga katika maandishi yake anasema kuwa nyuma ya mwaka 1970 akiw a mwanafunzi wa sekondari huko mkoani Kilimanjaro akisoma shule ya bweni. Shuleni hapo walikuwa wakisoma wanafunzi wa makabila mabalimbali wakiwamo pia Wasambaa kadhaa.
Kama ilivyokuwa wakati wa ujamaa kutoa nafasi ya vijana wengi kusoma sekondari nje ya mikoa yao ya asili. Kwa hiyo katika shule aliyosoma A. J Mshihiri walikuwepo vijana kadhaa Wakisambaa ambao walikuwa wakitokea Lushoto Tanga.
A.J. Mshihiri anasema kuwa wakati huo mawasiliano baina ya mwanafunzi na ndugu zake na marafiki nyumbani yalikuwa yanafanyika kwa kutumia barua. Anayeandika barua akishafanya hivyo alituma kupitia posta na mhusika hupata barua yake kwa sanduku lake la barua.
Ndiyo maana kwa wakati huo wale waliokuwa hawatambui kusoma na kuandika walikuwa wakitazamwa kuwa watu duni ambao walikuwa wakishindwa hata kuficha baadhi ya siri zao.
Ndugu A. J Mshihiri anadai kuwa zilifika barua shuleni na zikasomwa majina wa waliotumiwa. Siku hiyo A. J Mshihiri hakujaliwa kuwa na barua, lakini kijana mmoja mwenzake wa Kisambaa alipata barua kutoka huko Lushoto Tanga.
Kijana huyu kwa kuwa alipata barua hiyo, A. J Mshihiri anasema kuwa aliporudi bwenini alisoma barua yake na kupokea ujumbe kuwa alikuwa amefiwa na mama yake mzazi.
“Tulimsikia akilia na kutujulisha juu ya msiba huo wa mama yake mzazi, wanafunzi tulilijadili jambo hilo na tukakubaliana kuwa tumchangie kiasi cha fedha ambazo zilimtosha kwenda msibani Lushoto Tanga na kurudi Kilimanjaro, tulimkabidhi ndugu yetu huyu fedha hizo na yeye kuelekea safari ya msibani.”
Alifika Lushoto na kabla hajafika nyumbani kwao, punde aliposhuka tu kituo cha basi cha kijiji chake alikutana na kaka yake. Alimuuliza vipi mbona muda wa kufunga shule bado na unarudi nyumbani kufanya nini? Ndugu huyu alimwambia kaka yake kuwa nilipokea barua ya juu ya mama kufariki dunia. Huku akimuonesha barua hiyo ambayo alikuwa nayo.
Kaka yake alipoisoma alimwambia kuwa mama hajafariki na ametoka asubuhi kwenda shambani. Ndugu huyu hakuamini, kwa hiyo walimfuata shambani na huko hawakumkuta bali alikuwa amerudi nyumbani kuandaa chakula cha jioni.
Walipofika nyumbani wakamkuta mama yao yupo huku akianda chakula cha jioni cha siku hiyo, wakamueleza kilichotokea ujio wa mwanawe kutoka shuleni.
Walitazama vizuri barua hiyo, huku ikiwa na jina la aliyeandika, jambo hilo lilipelekwa kwa wazee wa eneo hilo na kuwajulisha viongozi wa kijiji hiki na kulijadili jambo hilo lililotokea huku wakimuita aliyefanya uchuro huo.
Katika kikao cha kijiji hicho miongoni mwa rafiki wa ndugu huyu aliyepewa barua ya msiba aliungama kikaoni kuwa ndiye aliyeandika, ila saini yake hakuweka na alifanya hivyo kama utani tu kwa kuwa mwandishi wa barua hii alikuwa MKINAKITUI na mwandikiwa alikuwa MKINASEUTA.
Wazee wa kijiji hicho walimkanya aliyeandika barua hiyo wakisema kuwa alilolifanya ni uchuro pia limemtia hasara kwa gharama mwezake kutoka Kilimanjaro hadi Lushoto.
Kikao cha wazee hao kiliamua ndugu huyo auze mifugo yake amlipe ndugu huyu fedha kama gharama za usafiri.Kweli hilo llifanyika. Kijana huyu akarudi zake shuleni ambapo alikuwa akisoma na A.J. Mshihiri na kuwasimulia kilichotokea
Je kipi kitaendelea?
Mwanakwetu subiri matini ijayo.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments