Header Ads Widget

WAKEREWE NA UDUGU WA DAMU

 


Adeladius Makwega

DODOMA.


Wakerewe ni kabila lenye mchanganyiko mingi wa watu walio na asili tofauti, ushahidi mkubwa unadai kuwa Wakerewe ni watu wenye asili ya Uzinza ambalo leo hii ni enero lilolopo katika Mkoa wa Geita ambao zamani ilikuwa ni wilaya ya Geita.


Wengine wakisema kuwa baadhi ya Wakerewe wanatokea huko Buhaya na Majita kama nilivyoeleza kwa kirefu nilipokuwa nasimulia utani baina ya Wajita na Wakerewe. Pia wengine wakitokeo huko Shangiro-Bukoba. Wakerewe hawa waliotokea Shangiro Bukoba ndiyo familia ya Chifu wa Wakerewe hadi ulipoondolewa uchifu katika Tangayika huru mwaka 1962.


Ikiaminika kuwa Wajita walikimbilia Musoma na Ukerewe mara baada ya kuibuka kwa njaa kubwa huko kwao na kufika Ukerewe.


Huo mchanganyiko maalumu ndiyo ukaibua kabila la Wakerewe ambalo kwa awali kabila hili lilikuwa ni jina linalotambulisha eneo tu la visiwa hivyo kuliko kusema kabila ambalo linataja mahusiano ya damu.


Wakerewe hao sasa wanaundwa na koo 15 ambazo ni Abasilanga ambao ndiyo ukoo wa chifu wa Wakerewe, Abasita (Abagwe), Abasiba, Abazuma, Abasi, Abahila, Abazigana, Abamile, Abagamba, Abasonge, Abaluhu, Abayange, Abahembe, Abazimu, na Abahimba.


Katika maandishi yaliyoandikwa na C.M.K Magogo juu ya Utani kwa kabila la Wakerewe, ndugu huyu anasema bayana kuwa kabila hili lina sifa moja kubwa ya kuwa ni wasiri mno katika mambo yao, kwa hiyo kuyafahamu inahitaji kazi kubwa.


Japokuwa kabila hili limekuwa wasiri mno juu ya mambo yao wenyewe wamekuwa na misemo kadhaa juu ya ndugu kutokuishi pamoja au kusaidiana mathalani methali kadhaa za kabila hili.

“Ologanda kalukana bala tilusuba nkiemo” 

na 

“Ahoe Abengi baba oturangu tebulato.”


Hapa wakimaanisha kuwa familia na ukoo unavozidi kuongezeka ndivyo udugu unavyopotea kabisa. Wakerewe wanaenda mbali zaidi wanasema ndivyo matatizo yanavyokuja katika ukoo.


Hili maana yake kubwa ni kweli ukoo unavyozidi kuwa mkubwa ndivyo wana ukoo wanavyotawanyika kutafuta ardhi na rasimali nyingine mbali na kwao. Kwa mfano ukoo wa Abasilanga ukaelekea Usukumani wakiwa na kiongozi wao aliyefahamika kama Matambo. 


Ndiyo maana Wasukuma wa Nasser ni Watani na Wakerewe (Wasilanga) kwa sababu Wasilanga ni watoto wao ambao waliokimbilia Usukumani kwa sababu ya kukua kwa koo hiyo. Huku Wasilanga wakisema kuwa hiyo siyo sababu ya utani wao bali Wasukuma waliwahi kuoa binti wa Wakerewe (Wasilanga)


Udugu katika kabila la Wakerewe upo kwa ndugu wanaozaliwa baba na mama mmoja lakini udugu wa damu upo baina ya wale wanaozaliwa na baba mmoja lakini mama mbalimbali. Hawa huwa ni ndugu wa damu kabisa. Wale wa baba na mama mmoja huitwa BW ‘OBUNENE na ule wa baba mmoja na mama tofauti uitwa OLWOSE BW OBUNESE.


Katika kabila hili kumekuwa na misemo kadhaa juu ya udugu huu wa damu ambao unatazamwa kuwa pia unaleta uadui mkubwa. Kwa jamii nyingi za kiafrika udugu wa damu unatazamwa kuwa unaleta umoja, japokuwa ndani yake kuna matatizo mengi.


“Obunese butekezanya ensegate.”


Wakimanisha kuwa ndugu hawa hawawezi kuishi pamoja au kukaa pamoja.


Wakerewe wanao pia msemo mwingine.


“Olwose lwobunene tiluangya ensoga”


Hapo wakimaanisha kuwa ndugu hawa hawezi kunywa pombe pamoja.


Kwa hakika misemo hiyo ya Wakerewe ndiyo ukweli wa mambo, familia nyingi za kichifu mara baada ya kufariki wazazi wa watoto wao waliobaki walingia katika migogoro mikubwa ya kugombea uchifu na kufarakana mno.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS