TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Ndugu waandishi wa habari, awali ya yote tunapenda kutoa shukrani kwa wadau mbalimbali wa usalama barabarani bila kuwasahau waandishi wa habari kwa namna ambavyo mnaendelea kuunga mkono jitihada za kudhibiti matukio ya ajali nchini.
Hali ya usalama barabarani inaendelea kuwa shwari na hakuna matukio makubwa ya ajali yanayotishia usalama wa watu na mali zao wanapokuwa barabarani.
Ndugu waandishi; tumewaita kwa lengo la kutoa ufafanuzi kuhusiana na picha zinazoonyeshwa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha baadhi
ya mabasi yanayofanya safari zake kutoka kituo cha mabasi cha Magufuli jijini DSM kuelekea mikoa ya kaskazini. yameegeshwa pembeni mwa barabara itokayo Dar es salaam kuelekea Moshi katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kuzuiwa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wa kituo cha Same kwa kuwahi kufika wilaya ya Same kinyume cha utaratibu.
Kilichotokea ni kwamba mnamo tarehe 03.02.2022 mchana huko Wilaya ya Same maafisa wa LATRA Mkoa wa Kilimanjaro walikuwa katika kazi ya ufuatiliaji wa mabasi ya abiria yasiyozingatia ratiba za usafiri wa mabasi (timetable) kutokana na hali hiyo madereva wa mabasi kwa hofu ya kuchukuliwa hatua waliamua kuegesha mabasi pembeni mwa barabara wakisubiri muda wa kufika check point
ya Same ambao kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na LATRA wanatakiwa kufika Wilaya ya Same saa 7:30 mchana na mabasi hayo yalifika eneo la KIRINJIKO majira ya saa 6:35 mchana na umbali uliopo kati ya KIRINJIKO eneo yalipogeshwa mabasi hayo na SAME ni takribani KM 20.
Wakati mabasi yakiwa yamepaki katika eneo hilo ndipo mtu mmoja ambaye hajafaamika alipiga picha na kutoa shutuma nzito. Katika eneo la KIRINJIKO hakukuwa na askari wa usalama barabarani aliyezuia magari hayo yasiende Same.
Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani tutaendelea kusimamia sheria kanuni na taratibu za usalama barabarani zinazosaidia kuwadhibiti madereva wanaokwenda mwendo unaohatarisha maisha ya watu na mali zao.
Makosa hatarishi kama vile mwendokasi na kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhali (wrong overtaking) tutaendelea kuyadhibiti kwani ndiyo yanachangia kutokea kwa ajali nyingi za barabarani nchini na tunawaomba madereva wote tushirikiane katika hili kwani ajali zinaweza kuepukika na kuzuilika endapo kila dereva atazingatia sheria za usalama barabarani, madereva wa mabasi ya abiria wanakumbushwa kuzingatia kwenda mwendo wa Km 50 kwa saa kwenye makazi ya watu na mwendo usiozidi Km 80 kwa saa kwani hayo ni matakwa ya kisheria.
Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani tutaendelea kushirikiana na mamlaka zingine zinazohusika na upangaji wa ratiba za mabasi ili kuwa na ratiba za mabasi zinazozingatia hali halisi ya barabara lakini bila kuathiri sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.
MWISHO;
Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani tunawakumbusha madereva wote
kuwa makini katika kipindi hiki cha mvua zinazosababisha utelezi barabarani wazingatie sheria.
“JALI MAISHA YAKO NA YA WENGINE BARABARANI”
traffic.hq@tpf.go.tz traffichqdar@gmail.com
0 Comments