Wangindo ni kabila mojawapo linalopatikana na katika mikoa ya Lindi, Morogoro, na Pwani, hapo awali lilikuwa likipatikana katika mkoa unaofahamika kama Mkoa wa Kusini sasa ndiyo mkoa wa Lindi. Ndugu hawa wanapatikana mno katika eneo la Madaba, Ndapapata, Kibata, Mbemkulu, Ngarambe, Ilonga, Kibaha na liwale.Mwandishi Adeladius Makwega-DODOMA
Huku Liwale ikifahamika kama ndipo makao makuu ya Wangindo wengi ndiyo kusema Liwale ndiyo Boma la Wangindo.
Unapoitazama asili ya Wangindo kumekuwa na simulizi kubwa mbili.
Kwanza ni SIMULIZI YA MAGENGU. Simulizi hii inadai kuwa ndugu hawa walikuwa wakijishugulisha mno na kilimo cha mahindi, mtama, uwele na viazi vitamu huku asili yao ni maeneo ya Madaba, Liwale na Ndapapata, hawa wakiaminika ndiyo Wangindo asilia.
Wakimaliza kulima iliaminika kuwa walikuwa wakiwinda wanyama mbalimbali. Wakiwa huko walijishughulisha na ulinaji wa asali. Huko misituni walikutana na wadudu wadogo wadogo kama nyuki ambapo wao waliwaita ITAPALUKU.
Wangindo hao walitafuta hata asali katika mapango ambayo waliyoyaita kama MBAKO.
Kwenye Mbako kulikuwa na asali inayotengenezwa na Itapaluku iliyofahamika kama KICHOMA.
Walipokuwa wakienda kulina asali hiyo Wangiido hawa hawakuvaa mavazi yoyote yale, huku nyuki hao hata kama waliwauma hawakusikia maumivu yoyote, ikiaminika kuwa walikuwa na dawa maalumu ya kupambana na nyuki.
Walikuwa wakisafiri umbali mrefu mno kutafuta maji, bila ya kujali maji yapo wapi, kubwa kwao ilikuwa ni upatikanaji wa asali na nyama tu.
Asili ya pili ni ya SIMULIZI YA NDWEWE hawa ni Wangindo kutoka kata moja inayofahamika kama Ilonga, Wilaya ya Ulangam mkoani Morogoro. Inaaminika kuwa hawa ni miongoni mwa masalia ya Wangoni kwa kiongozi anayefahamika kama MACHONDA. Wakiwa na simulizi sawa na Mbunga ambao nao ni masalia ya Wangoni.
Tofauti kati ya MBUNGA na NDWEWE ni kuwa akina Mbunga bado hadi sasa wanazungumza Kingoni lakini hawa Wandewe (Wangindo wa Ilonga ) wao walioana na Magengu kwa hiyo wakapoteza asili yao ya Ungoni na hadi sasa wanazungumza Kingindo.
Wandewe wanapozungumza Kingindo huwa maneno yao hawawekei msisitizo. Wangindo hawa wa Ilonga, binafsi mimi ni ndugu zangu kabisa, kwani awali kata hiyo ya Ilonga mababu zangu walikuwa wakiitika hapo. Sasa ni sehemu ni Kata ya Ketaketa yenye vijiji vya Luhombero, Ikangao na Ketaketa. Mimi asili ya kwetu ni Kitongoji cha Mrundu (kilichozaliwa na jina la Mto Mrundu), katika Kijiji cha Ikangao(Kinachotokana na Mto Ikangao) maji yote yakimwagwa Mto Luhombero.
Huku Ketaketa na Ilonga zikiwa ni kata za Wilaya ya Ulanga kwa sasa zikiwa na makabila ya Wapogoro wengi na Wangindo(Waliopelekwa hapo na Mwingereza).
Kata hizi zipo jirani kabisa na Mbuga Selous na jirani na mpaka wa mikoa ya Morogoro na Lindi.
Kabila la Wangindo wanapatikana mno katika maeneo mbalimbali kama vile KIlwa Njinjo, Kidodi, Mahenge, Kisaki, Ifakara, Kilombero, Rufiji na wengine wakiishi huko Kibaha kama nilivyokujulisha ukiwa n mtawanyiko maalumu ndani ya mkakati wa Mjerumani.
Wakati wa vita vya maji maji Wangindo ni nimojawapo la kabila liliokuwa korofi mno kwa utawala wa Mjerumani na baadaye Mwingereza. Jambo hilo liliwafanya Wajetumani walihangaika mno, huku mbinu ya kulitawanya kabila hilo ikiwa suluhu.
Idaiwa Wangindo wakiwa chini ya Kiongozi wao aliyefahamika kama Hongo hali ilikuwa tete kwa Wajerumani na walihisi kuwa kunaweza kuibuka vita vingine katika eneo hilo baada ya MAJIMAJI.
Kumbukumbu za Wajerumani zilionesha ukorofi huo wa Wangindo kama anavyoandika mtafiti Kuchimwa Jurando katika maandishi yake ya Utani Relationship:The Ngindo 1975.
WAkati wa kusudio hilo la kuwatawanya Wangindo, Mjerumani alifurushwa na Mwingereza baada ya kushindwa Vita vya Kwanza vya Dunia. Mwanakwetu maandishi yanadumu, kwa hiyo Mwingereza alibaini hilo katika kumbukumbu za Mjerumani.Tabia ya udhalimu haikubadilika, bali jina na mkoloni ndilo lililobadilika
Kwa usalama wa Mwingereza aliwatawanya Wangindo katika makundi makubwa mawili, kundi la kwanza walipelekwa huko Njinjo Kilwa, na kundi lengine lilipelekwa huko Ilonga Ulanga-Morogoro kwa wale ndugu zangu niliowataja hapo awali.
Sasa hawa Wangindo waliopelekwa Njinjo Kilwa walikumbwa na balaa la njaa kubwa na safari yao ya uhamisho iliendelea hadi Kibaha kuokoa maisha yao. Kwani eneo la Kilwa Njinjo hata leo ni eneo ambalo lina ardhi isiyo na rutuba sana.
Sababu ya pili eneo hili la awali la Wangindo lilikumbwa na Homa ya Majano-Malale na jambo hilo lilisababisha Wangindo wengi kufariki, huku wengine waliosalia kuondoka eneo hilo.
Mwanakwetu umeielewa simulizi ya Wangindo? Je kabila lako simulizi yake inavutia kama ya Wangindo?
Subiri matini ijayo.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments