MBUNGE wa viti maalum (CCM) kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri amewataka wanawake wa chama hicho kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hasani kwa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama.
Zuena alitoa kauli hiyo katika mkutano mkuu maalum wa chama wilaya ya Moshi mjini ambapo alisema kuwa, Rais Samia amefungua milango kwa wakinamama kuwania nafasi na uongozi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na kujiamini.
Alisema kuwa, wanawake ni jeshi kubwa ambalo wakiamua wanaweza na kuwataka kumuunga mkono kwa kujitokeza kwa wingi kugombea katika nafasi mbalimbali.
"Mwenyekiti wetu ameonyesha kuwa wanawake tunaweza kuongoza hivyo tunajukumu la kufwata nyayo zake kwa kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi" alisema Mbunge Zuena.
Akizungumzia swala la Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu, Zuena aliwataka kutoa ushirikiano ili kuhakikisha serikali inapata takwimu kamili.
Alisema kuwa, lengo la serikali kufanya sensa ni ili kupata takwimu kamili na kuweza kuwahudumia wananchi wake kulingana na idadi.
"Niwaombe wakinamama tuachane na tabia ya kuwaficha watu wenye ulemavu na wazee kwani nao wanahaki zao ambazo serikali inapaswa kuwatekelezea hivyo tusiwafiche" alisema Zuena.
0 Comments