Header Ads Widget

KISARAWE KWENDA KIBAHA (III)

Mwanakwetu naamini u mzima kabisa na unaendelea na kazi za kila siku. Kwa leo nataka tutafakari pamoja juu ya suala la maendeleo na mchango wa kila kiongozi katika maeneo aliyokabidhiwa iwe kwa barua, kura au kwa wale wanaorithi.Mwandishi Adeladius Makwega


Majukumu makubwa ya kiongozi ni kuhudumu kwa maslahi ya walio chini yake na yeye mwenyewe kwa kuwa kiongozi ni sehemu ya jamii husika. ambapo yeye anayofanyia kazi ni kwa niaba yake na nduguze (jamii anayoiongoza).


Mathalani chifu akimtuma kijakazi wake akanunua bunduki na mishale kwa ajili ya kupambana na simba wakati wa hatari, aliyetuma anawajibu wa kununua bunduki sahihi na mishale sahihi ili siku adui simba akija watapambana naye vizuri.


Kinyume chake akinunua bunduki ambayo mbovu na mishale yenye nguvu hafifu simba akija atawala nyama yoyote atakayemkuta kama aliyekwenda nunua, hata chifu mwenyewe au hata mtu wa kawaida. Kwa kuwa waswahili wanasema NYAMA, NYAMA NYAMA! 


Leo tena ninaendelea na habari juu ya Kijiji cha Kimara Misale ambacho sasa nimeambiwa kimehamishiwa Kibaha Vijijini, Kijiji hiki ni cha mwisho katika mkoa wa Pwani kinapakana na mkoa wa Morogoro. Tangu ukoroni wa Mjerumani kijiji hiki kilikuwa ndani ya Wilaya ya Kisarawe na awali kabla ya mkoroni kwa desturi ndugu hawa walikuwa wakivuka Mto Ruvu kwa kutumiwa ngalawa kwenda kwa ndugu zao wa damu wa Mzenga, Bembela na Kisarawe.


Waliowahi kuwa Wabunge wa Kisarawe mpaka sasa ambao ni wazaliwa wa ukanda huu ni Athumani Janguo na Selemani Jafo. Kwa Profesa Kighoma Malima alikuwa Mbunge wa Kisarawe lakini yeye alikuwa ni mzaliwa wa Mkamba ambayo sasa ni sehemu ya Wilaya ya Mkuranga.


Ebu nikurudishe nyuma zaidi msomaji wa matini hii, kwa wanyeji wa Dar es Salaam hapo awali watakumbuka kituo cha mabasi ya kwenda bara kilikuwa Kisutu na Mnazi Mmoja, huku baadhi ya mabasi hayo yakipakia abiria katika ofisi zao ambazo zilikuwa zimetapaka kati ya maeneo ya Kisutu na Kariakoo.


Baadaye kikajegwa kituo cha mabasi cha Ubungo ambapo hapo awali ilikuwa ni sehemu tu ya mabasi ya UDA(Usafiri Dar es Salaam). Mwaka jana 2021 kituo cha mabasi cha Ubungo kikahamishiwa Mbezi, mara baada ya kituo kikubwa cha mabasi cha Magufuli kukamilika.


Kwa wale ndugu zangu waliojaliwa kuwa na umri mkubwa watakumbuka kuwa eneo la Ubungo kabla ya kuwa kituo cha mabasi hali ilikuwaje ya maendeleo na maeneo eneo jirani na hali ilivyobadilika baada ya kituo kuanza kufanya kazi.


Hali hiyo inashabiana fika na hali ya Mbezi mara baada tu kuanza kwa ujenzi wa kituo hicho cha mabasi cha Magufuli. 


Je mwanakwetu umeshawahi kujiuliza kwa nini vituo hivyo vya mabasi vilianzia Kisutu na Mnazi Mmoja? na baadaye Ubungo na sasa Mbezi?


Mwanakwetu nakuuma sikio kuwa zamani sana barabara iliyokuwa inaenda Morogoro ilikuwa ni Barabara ya Pugu (Barabara ya Nyerere). 


Kwa faida ya msomaji wa matini yangu nakuuma sikio kuwa Barabara Pugu ndiyo iliyokuwa Barabara ya Morogoro zamani. Basi lilikuwa linatoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam liliingia Barabara ya Pugu moja kwa moja hadi Pugu lilipanda hadi Kisarawe, Kola, Mzenga, Mafisi hapo Mjerumani aliweka Pantoni watu walivuka na kuelekea Morogoro.


Ukivuka Mafisi walifika Kimara Misale, Geregete, Matuli, unaenda mpaka unatokea Uluguruni kwa Chifu Kingalu sasa hiyo ilikuwa Morogoro. 


Mwanakwetu hapa narudi tena kwa msisitizo kuwa ukitokea Mzenga, unapita Bembela, alafu Mafisi, hapo unafika kitongoji cha Pantoni ambacho sasa kimebaki jina kwani hakuna pantoni tena. Ukivuka hapo unaingia Kimara Misale sasa hapa ni kijiji cha mwisho cha mkoa wa Pwani.


Kimara Misale wanapakana na kijiji cha Usungura hapo kuna Mto Ngerengere ambapo kwa wakazi wa Kimara Misale huwa wanavuka kwa magogo kwenda upande huo wa pili.


Kwa maelezo ya wakaazi wa kitongoji cha Pantoni wanadai kuwa kivuko kilikuwapo, kwanza injini iliharibika baadaye wanadai injini Iliibiwa na kivuko kutokufanya kazi tena, huku wengine wakisema kuwa hata mabaki ya kivuko hicho yalizama na maji katika Mto Ruvu.Sasa ikawa mwendo wa kuvuka kwa ngalawa..


Wanakijiji wa Kimara Misale wanasema kwamba viongozi wa mwanzo wa Mkoa wa Pwani (Wakati wa Mjerumani) wakiwamo viongozi wa kimila walizembea kwani maeneo mengi yanayopitiwa na mito mikubwa kwa majirani zao Waluguru na Wapogoro walijengewa madaraja makubwa, kwanini eneo la Pantoni lilibaki na kivuko pekee? Wakati njia hiyo ilikuwa inaunganisha Pwani na Marogoro? 


Wakazi hawa wanasema kuwa wale waliokuwa viongozi wa kimila wa ukanda huo wa mwanzo hawakuchangamka kama walivyokuwa wenzao wa Morogoro.


“Wenzetu walichangamka mno, ukienda Morogoro picha hii unaweza kuiona vizuri, hali ya ujenzi wa madaraja yalivyokuwa makubwa na yalivyoungasha upande mmoja wa mto na upande mwingine.”Anasema Ali Mangala mkaazi wa Kimara Misare


Binafsi nasema kuwa mathalani Mjerumani angelijenga daraja kama yale ya Morogoro ya kabla ya Tanganyika huru eneo hili la Pantoni hali ingekuwaje?


Ndiyo kusema kwa hesabu za maendeleo ya Ubungo unayoiona leo, Mbezi unayoiona leo, Kibaha unayoiona leo, Mlandizi unayoina leo na Chalinze unayoina leo pengine ingekuwa upande huu wa Kisarawe kuekea Ngerengere hadi Morogoro Mjini ikipita kandokando ya reli ya uhuru.



Kwa hiyo kama kuna mtu mmoja tu alizembea wakati huo na mambo yakabadilika kabisa, kubwa wale ambao ni viongozi wa kuchaguliwa, kurithi na hata wale wa kupewa barua wajitahidi kutimiza wajibu wao vizuri.Isije ikawa kama hili la ndugu zangu wa Kimara Misale waliohama Wilaya Kutoka Kisarawe kwenda Kibaha.


Mwanakwetu nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com

0717649257.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI