Na Mwandishi Wetu
BUKOBA
Waendesha pikipiki za kusafirisha abiria maarufu kama bodaboda katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, wamesema hatua ya serikali kutunga sheria na kupitisha kanuni za ushuru wa maegesho bila kuchukua maoni yao ni uonevu kwao, maana inachangia kuongeza ugumu katika utendaji wa shughuli zao za kila siku.
Wakizungumza na vyombo vya habari bodaboda hao akiwamo Slyvery Slyvester wamesema kuwa kama serikali kupitia kwa Wakala wa barabara Mijini na Vijijini - TARURA - imeamua kuwatoza ushuru wa maegesho, wangewawekea utaratibu ambao utawafanya kulipa kwa mwaka, badala ya huu wa sasa ambao unawataka kulipa shilingi 300 kila siku.
"Tunakubali kulipa ushuru huu hatupingani na serikali, lakini tupewe utaratibu ambao hautatuumiza tulipe hata kwa mwaka ingawa kiasi hiki kwa siku bado ni kikibwa kwetu ikilinganishwa na kipato chetu" amesema Slyvester.
Mwendesha bodaboda mwingine Adulashiru Haruna amesema kuwa Rais wa awamu ya sita Samiah Suluhu Hassan alipunguza malipo ya adhabu ili kuwapatia unafuu wa maisha lakini alichokiondoa kimerudishwa kwa sura nyingine na kuwafanya kuendelea kuumia.
Kwa upande wake Paschale Augustine ambaye ni dereva wa taksi katika manispaa ya Bukoba, amesema awali walikuwa wanalipa shilingi 500 kwa siku lakini sasa wameongezewa hadi shilingi 1,000 kiwango ambacho wanaona ni kikubwa kulingana na hali ngumu ya sasa ya biashara.
Akitoa ufafanuzi kuhusu ushuru huo wa maegesho meneja wa Tarura katika wilaya ya Bukoba mhandisi Andondile Mwakitalu amesema kuwa upo chini ya sheria ya serikali za mitaa ya mwaka 1982, ambayo imetungiwa kanuni na kupitishwa na waziri wa Tamisemi Desemba 2021, na kwamba utekelezaji wake umeanza Februari 07 mwaka huu.
"Wanachopaswa kukifanya wamiliki wa vyombo vya moto ambavyo ni magari, bajaji na pikipiki ni kutoa ushirikiano kwa kulipa ushuru huu maana upo kwa mujibu wa sheria, kuliko kushindwa kutii sheria wakaanza kukimbizana kuwakamata na kuwatoza faini au kuwapeleka mahakamani" amesema.
0 Comments