BAADHI ya Wakazi wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wamekumbwa na taharuki kufuatia zoezi lililofanywa na Jeshi la zimamoto na uokoaji la Mkoani humo la kuzima moto kwenye Benki ya NMB Tanzania tawi la Songea ......................NA AMON MTEGA,SONGEA
Akizungumza mmoja wa wakazi hao Faustin Msemwa amesema kuwa zoezi hilo ambalo limefanyika Februari 11 mwaka huu majira ya saa 05:00 asubuhi liliwashitua watu wengi ambao waliamini kuwa benki hiyo inawaka moto jambo ambalo baadhi yao walikuwa wakiwazia fedha zao.
Msemwa amesema kuwa zoezi hilo licha ya kuwaletea taharuki lakini bado limewasadia kuwapatia elimu ya namna ya kukabiliana na majanga ya moto ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.
Hata hivyo mkazi huyo ameliomba Jeshi la zimamoto na uokoaji kuongeza visima vya maji katika Manispaa ya Songea ili kufanikisha kukabiliana na majanga ya moto kwa haraka zaidi .
Kwa upande wake Meneja huduma kwa wateja wa Benki ya NMB tawi la Songea Mwalimu Mbwambo amesema kuwa zoezi hilo lillilofanywa na Jeshi la zimamoto na uokoaji limeshirikisha taasisi mbalimbali ikiwemo ya Afya ambapo kila taasisi imeshughulika kwenye nafasi yake.
Mbwambo ambaye pia ni kaimu meneja wa benki hiyo amesema kuwa zoezi hilo halikuwa kwa taasisi hizo pekee bali ni pamoja na kutoa elimu kwa wakazi wa Songea juu ya kukabilina na majanga ya moto pindi yanapotokea .
Katika zoezi hilo elimu mbalimbali imetolewa ikiwemo ya namna ya kuwaokoa watu waliopo kwenye hatari ya moto pamoja na utumiaji wa maji wakati wa kuzima moto .
.
0 Comments