WATU watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Pwani kwa tuhuma za kuvunja kiwanda cha kukamua alizeti na kuiba mota 13 zenye thamani ya shilingi milioni 77.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani Pwani (ACP) Wankyo Nyigesa alisema kuwa kiwanda hicho ni mali ya wajasiriamali wawili.
Nyigesa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 22 mwaka huu majira ya saa 10:45 huko Misugusu kata ya Misugusu wilaya ya Kibaha kwenye kiwanda cha Patrick Sungura (65) mkazi wa Kibamba na Fredrick Chacha (32).
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Nicolaus James (28) fundi mota mkazi wa Mbagala, Makoye Athuman (46) fundi magari mkazi wa Kimara Matosa na Machea Mzamilo (21) fundi mota mkazi wa Kimara.
"Baada ya upelelezi wa kina na taarifa za kiintelijensia Polisi liliwakamata watuhumiwa hao na walipopekuliwa katika makazi yao walikuwa na mota hizo 13," alisema Nyigesa.
Pia Jeshi hilo linamshikilia mtu ambaye jina lake limehifadhiwa akiwa na pikipiki kikiwa na vipande 37 vya nyaya ambazo zinadhaniwa ni kutoka katika miradi inayoendelea kujengwa mkoani Pwani.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 24 mwaka huu majira ya saa 11:30 huko Kijiji cha Mdaula kata ya Ubena ambapo Polisi walikamata pikipiki yenye namba za usajili Mc 275 Bey aina ya Sanlg.
Aidha alisema kuwa Jeshi hilo limefanya misako mbalimbali kuanzia Januari 15 hadi 27 na kukamata jumla ya watuhumiwa 63 huku wanaume wakiwa 53 na wanawake 10.
"Misako hii ni kudhibiti makosa ya uvunjaji, unyanganyi wa kutumia nguvu, wizi, wizi wa mifugo, utumiaji wa dawa za kulevya na matumizi ya pombe haramu ya Moshi ambapo watu hao walikamatwa na vitu mbalimbali,"alisema Nyigesa.
Alibainisha kuwa wanatoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi kwa kutoa taarifa za uhalifu na pia wajitokeze pale wanapoibiwa ili kutoa ushahidi.
Mwisho.
0 Comments