Na Mwandishi Wetu,
Arusha.
Wakazi wa Jiji la Arusha wamekumbushwa kufuata taratibu wa kisheria za Mipango Miji kabla ya kuanza ujenzi wowote wa majengo ili kuepuka changamoto ya ujenzi holela unaochangia kuharibu taswira ya mji.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Moshono katika wiki ya sheria iliyoandaliwa na Jiji hilo, Afisa Mipango Miji Julius Kiabona amesema ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kujenga bila kufuata utaratibu wa ujenzi ambao unamtaka mhusika kufika ofisini kwa ajili kujua taratibu hizo ambazo ni pamoja na kujzaa fomu maalumu ya kuomba kibali cha ujenzi.
Amesema kwenda kinyume na utaratibu huo kumesababisha malalamiko kutoka kwa wananchi baaada ya nyumba zao kuwekewa alama X inayomtaka kusimamisha ujenzi ili kufuata taratibu za ujenzi na kwamba elimu hii hutolewa kila mara na ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji kupitia mikutano na matangazo mbalimbali.
“Utaratibu unakutaka kuchukua fomu ya kuomba kibali ofisi za jiji au ofisi za Kata, na haya kama kiwanja chako hakijapimwa utapewa kibali cha ujenzi ambapo baada ya kuijaza utaiambatanisha na ramani yako ya ujenzi, lakini ukienda kinyume utawekewa X na utatakiwa kulipwa faini pia" Alisema Kiabona.
Aidha Kiabona alitoa elimu ya hati miliki na leseni ya makazi kwa wananchi hao kwamba ndiyo nyaraka halali zinazotambulika kisheria na kuwataka wananchi hao kuwa na hati moja kati ya hizo kabla ya kuanza ujenzi kwani sheria haitambua hati ya mauziano ya watu wawili.
“Watu wamekuwa wakitumia hati za mauziano kujenga bika kuwa na hati miliki au leseni ya makazi na ndiyo maana unaona ujenzi holela, niwatahadharishe tu kuwa hati hizo hazitambuliki kisheria hivyo unatakiwa kutafuta hati miliki au leseni ya makazi ili uwe na uhalali wa kumiliki kiwanja chako kisheria.
Amesema Jiji la Arusha lina Mpango Kabambe wa Ujenzi (Master Plan) ambao umeainisha maeneo ya ujenzi wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzingitia miundombinu yote kwa maana ya maji, barabara, umeme, shule, hospitali, viwanja vya mpira na zinginezo hivyo ofisi ya Mipango Miji itahakikisha hakuna mtu anaharibu mpango huo kwa kutofuata utaratibu.
Kwa upande wake Gabriel Laibon mkazi wa Kata ya Moshono ameshukuru kwa kupata elimu hiyo kwani hapo awali hakujua kuwa ili uweze kujenga ni lazima upate hati ya ujenzi kutoka ofisi za Jiji na sasa atakuwa balozi mzuri kwa wenzake.
"Hata hili la kuwa na hati miliki au leseni ya makazi ndo nasikia hapa, nilijua ukishanunua na mkaandikishana kumbe bado huna uhalali kisheria na eneo hilo, basi kwa elimu hii watu wengi tunakaa au kumiliki viwanja ambavyo siyo vyetu kisheria.
Wiki ya sheria katika Jiji la Arusha inaendelea ambapo wataalamu wake wa Sheria, Mazingira, Mipango Miji, Ustawi wa Jamii, pamoja na Idara ya Maendeleo ya Jamii wanatoa huduma za kisheria ikiwemo sheria ya ndoa, sheria ya ardhi, sheria ya mirathi na wosia, sheria ya Mazingira, Sheria ya Mipango Miji pamoja na kuelemisha jamii juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwenye jamii.
MWISHO.
0 Comments