NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Naibu waziri wa madini Dkt Steven Kiruswa amewataka viongozi mbalimbali wakiwemo wa Dini na kimila kufikisha ujumbe wa umuhimu wa sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika August mwaka huu ili wananchi waweze kutoa ushirikiano na taarifa sahihi ili kufanikisha azma ya zoezi hilo.
Dkt Kiruswa aliyasema hayo katika semina ya sensa ya watu na makazi iliyotolewa kwa viongozi wa dini na Kimila ambayo imeandaliwa na taasisi ya Kiislamu inayofuata maadili aliyoagoza mwenyezi Mungu(TWARIQA)ambapo alisema kuwa sensa hiyo itasaidia upatikanaji wa takwimu itayosaidia Dora ya maendeleo ya taifa.
Alisema kuwa sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi kwa umri na jinsia,mahali wanapoishi, Hali ya Elimu, ajira, vizazi, vifo, makazi ambapo misingi hiyo ndiyo inayoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi Makundi maalum yenye uhitaji maalum kama vile watu wenye ulemavu, watoto, wanawake, vijana na wazee.
“Natambua viongozi wa dini zote Wana jukumu la kubwa la kuwa viungo kati ya serikali na wananchi na viongozi wa Mila ili kudumisha amani kupitia nyumba za ibada kwa kufundisha maadili mema kama vitabu vitakatifu vinavyoelekeza na Nina imani viongozi wote mliokuja Leo mnauwezi wa kuelimisha jamii kutokana na nyazifa zenu,” Alisema Dkt Kiruswa.
Alifafanua kuwa umuhimu wa sensa ni pamoja na serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia Mchakato wa utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa 2025, kuboresha huduma za kijamii, kutoa viashiria vya maendelo na kutolea mfano pato la mtu ambapo takwimu za sensa ya mwaka 2012 ilionyesha kuwa Idadi ya watu ni zaidi ya million 44, wanaume wakiwa ni zaidi ya milioni 21 sawa na asilimia 48.7 na wanawake zaidi ya milioni 23 sawa na asilimia 51.3, huku milioni 31 sawa na asilimia 70.1 wanaoishi vijijini na milioni 13 sawa na asilimia 29.6 wakiishi mijini ambapo kwa sensa ya 2022 inakadiriwa idadi itakuwa ni zaidi ya milioni 60.
Sambamba na hayo pia alisema kuwa katika sensa itayofanyika August mwaka huu wizara ya madini inatarajia kuweka dodoso litakalosaidia kukusanya taarifa za wachimbaji wa madini wakiwemo vijana na wanawake ili kuweza kujua mahitaji yao hivyo wachimbaji wote nchi nzima watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa zao kwa usahihi na za watu waliowaajiri.
Kwa upande wake Mratibu wa sensa mkoa wa Arusha Leokadia Athanas Mtey alisema kuwa sensa itasaidia serikali kupanga mipango mbalimbali ya kimaendeleo kwani inategemea takwimu katika kufanya shughuli za maendeleo ya nchi ambapo sensa hiyo itakuwa ni sensa ya 6 tangu nchi kupata Uhuru.
Alisema kuwa watu wanaostahili kuhesabiwa ni watu wote waliolala ndani ya mipaka ya Tanzania ambapo lengo kuu ni kuhakikisha kwamba kila mtu aliyelala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa anahesabiwa na atahesabiwa mara moja.
“Sensa inayoenda kufanyika ipo kiutaratibu na miongozo na taarifa zote binafsi za watu zitakazokusanywa ni siri na zitatumika kwa madhumuni ya takwimu tuu hivyo wananchi msiogope kutoa taarifa sahihi kwani wakitoa taarifa za uongo itafanya serikali ipange mipango ambayo haitakiwa na manufaa kwa wananchi,”Alisema Mratibu huyo.
Aidha alifafanua kuwa serikali wakati inapanga mipango yake, bila kuwa na taarifa sahihi hawawezi kujua wapi panahitaji jambo fulani au wapi Kuna changamoto zinazohitajika kutatuliwa ili wananchi waweze kufikia kimaendeleo hasa katika huduma za kijamii ambapo kwa mara ya kwanza sensa ya watu na makazi itafanyika kwa kwa kutumia vishkwambi tofauti na awali ambapo ilikuwa ikifanyika kwa kutumia makaratasi.
Naye Katibu wa Taasisi ya Twariqa Tanzania Yahaya Athman Mkindi alisema kuwa zoezi hili ni muhimu kwa kuwa inawasaidia serikali na wadau wengine,kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta ya mbali mbali kama elimu,afya,hali ya ajira,miundombinu ya barabara nishati na maji safi.
0 Comments