Header Ads Widget

MWANAKWETU NA MIMI NIMEMPONGEZA

 



Adeladius Makwega

DODOMA.


Januari 27, 2022 niliamka nyumbani kwangu kama zilivyo siku nyengine. Nilipofika kituo cha basi nilikutana na daladala ambayo nilipata kiti na kuketi na kuianza safari ya kuelekea huko kwa kina pangu pakavu tia mchuzi.


Daladala hiyo, abiria wake hatukuwa wengi sana lakini viti vyote vya basi hili vilijazwa. Tuliendea na safari kama dakika tano hivi, naye kondakta alipita na kuchukua pesa yake na mie kumlipa shilingi 1000 na kumuelekeza kuwa nimepanda Chamwino nashuka Mji wa Serikali.


Safari iliendelea, huku kwa mbali nikisikia katika redio kama sauri ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassani. Sauti hiyo nilibaini yupo katika kipindi kimojawapo cha TBC Taifa. Lakini baadaye nilitambua hakuwa TBC Taifa, bali alikuwa TBC 1. Hawa jamaa wa TBC Taifa niligundua kuwa walijiunga tu. 


Huku nikiwa katika daladala hiyo nilibaini kumbe TBC 1 walikuwa na mheshimiwa Rais kwani mheshimiwa huyu alikuwa akisherehekea sikukuu yake ya kuzaliwa Januari 27. 


Nikiwa katika basi hili niliona kila abiria yu kimya, tukisikiliza namna mheshiwa wetu akiongea. Binafsi nilikuwa kimya zaidi kusikiliza je kuna abiria yoyote atasema chochote juu ya siku ya kuzaliwa ya mheshimwa huyu?


Masikio na macho yangu yalikuwa kama mshabiki wa mpira ambaye timu yake imefungwa alafu timu yake inashambulia goli la adui.Nilikuwa kama shabiki aliyekodoa macho na kutega masikio yake kusubiri goli kuingia kimiani.


Lakini hilo sikulishuhudia mwanakwetu.


Mara nilimsikia Mheshimiwa Rais Sania akimtaja Musa Twangilo ambaye ni mtangazaji na mtayarishaji vipindi wa TBC kwa muda mrefu, nilikumbuka kuwa huyu ni Mzigua wa huko Tanga.


Nikiwa katika gari hilo nilimkumbuaka Musa Twangilo wa mwaka 2009 akitokea Chuo Kikuu cha Makerere Uganda. Akiwa Makerere alifahamika kama Musa Ali. Nilipokutana naye mwaka 2009 binafsi nilimuuliza kaka hauna jina la ukoo la kibantu, shemeji yangu huyu Mzigua alinijibu kuwa ukoo wao ni TWANGILO.


Nikamuomba atumie Musa Ali Twangilo, ndugu huyu alinijibu kuwa hili halipo katika vyeti, nikamwambia hilo ni jina lako la ukoo jaribu kulitumia, ndugu zako wa Uziguani wakisikia Musa Twangilo watafurahi sana. Kweli shemeji yangu huyu alitumia jina hilo la ukoo.


Daladala hii ikafika Mji wa Serikali na wakati nashuka nikasikia Mkurugenzi wa TBC Dkt Ayub Ryoba akimshukuru mheshimiwa Rais na kumtakiwa heri ya siku ya kuzaliwa. Nikajiuliza moyoni aha na yeye mjivuni yupo?


Nilimkumbuka mjivuni Dkt Ryoba akiwa mwalimu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam na wakati huo akiwa Mjumbe wa Bodi ya TBC mara baada ya kuundwa kwa Bodi mpya ya TBC na kumaliza muda wake wa bodi ya zamani ya TBC ya Profesa Mwajabu Possi.


Mjivuni huyu akiwa mjumbe wa Bodi ya TBC tulimuamini mno na tulimpongeza sana kwa pongezi tele, nilikumbuka kuna siku tulimfuata ofisini kwake chuoni angalau kumpa baadhi ya mambo yaliyokuwa yanawakwaza watumishi wa TBC.


Mwanakwetu safari hiyo niliingoza mimi nikiwa na mzee mmoja msataafu sasa anaitwa Malima Ndelema. Tulizungumza naye mengi mjivuni huyu, lakini kilichotokea nitakusimulia katika simulizi zangu zijazo. Haya yote niliyakumbuka nikiwa sasa naenda kwa akina pangu pakavu tia mchuzi.


Nilipofika kwa akina yakhe, nilikaribishwa na ujumbe wa kuombwa nitayarishe tangazo la pongezi la siku ya kuzaliwa mheshimiwa rais wetu, kweli nilifanya hivyo. Mara nilipata simu ya mheshimiwa mmoja nayeye akitaka nitayarishe tangazo la kumpongeza mheshimiwa na yeye nilimuunganisha na mtu akatengenezewa tangazo hilo la pongezi.


Baada ya saa moja alikuja jamaa mwingine akiomba nayeye nimtayarishie kibango juu ya mheshimiwa huyu kwa kuwa viongozi wenzake wa chama chao cha siasa wamekubalina kazi hiyo ifanyike haraka kabla ya saa 5 ya asubuhi ya Januari 27 ili wampongeza mheshimiwa rais.


Kumshauri ndugu yangu huyu ambaye alikuwa akiifanya kazi hiyo kwa niaba ya chama chake cha siasa nilimwambiwa mie sifahamu kutengeneza kibango hicho lakini nikaona ni busara kumshauri namna nyengine ya kumpongeza mheshimiwa rais wetu.


“Kumuandikia barua ya pongezi, kumtungia shairi, utenzi au wimbo, unaweza kumuandikia makala ya pongezi ikachapwa gazetini na nakala hiyo kuitumia kwa jina lake kwa njia ya posta.”


Ndugu huyu aliniambia kuwa anakwenda kuiandika barua ya pongeza ya siku ya kuzaliwa ya mheshimiwa rais wetu. Nikasema kimoyo moyo naona leo watu wako bize kumpongeza mheshimiwa rais wetu. Nikakumbuka kuwa na mimi sijampongeza mheshimiwa rais, ninangoja nini?


“Kwa heshima na taadhimu, nakupongeza sana, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani kwa siku yako ya kuzaliwa. Hongera sana Mama. Nakutakia maisha marefu-Allan wa Sahlan.”


Mwanakwetu sasa na mimi nimempongeza mheshimiwa rais wetu. Kama na wewe umechelewa kumpongeza kisa haukujua kutengeza kibango mwakani mwandike barua/tunga shairi -anza kutunga beti moja moja kila mwezi yenye mistari minne hadi ikifika mwakani una shairi  lenye beti 12 na hakika mheshimiwa wetu atasoma tu.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI