Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
SEKTA ya Utalii imeendelea kuimarika kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ikiwa juhudi za kupambana na Ugonjwa wa UVIKO19.
Hayo yasemwa leo Januari 29, 2022, Katika ukumbi wa Chuo cha Utalii cha Taifa (NCT) Kampasi ya Dar es Salaam, na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Massanja [MB] wakati wa uzinduzi wa mafunzo kwa watoa huduma za Utalii nchini kuhusu mwongozo wa kukabiliana na janga la UVIKO 19 katika sekta ya Utalii.
Naibu Waziri Mary Massanja alibainisha kuwa, kabla ya mlipuko wa janga la UVIKO 19, kuikumba dunia, sekta ya Utalii ilikuwa ikichangia takribani asilimia 17.2 ya pato la Taifa, asilimia 25 ya mauzo ya nje na asilimia 60 ya mapato yote yatokanayo na biashara za huduma nchini.
Aidha, ameongeza kuwa, sekta hiyo imekuwa ikichangia uchumi wa Nchi zaidi ya shilingi Trilioni 6.06. sawa na; [Dola za Marekani Bilioni 2.6] huku ikizalisha ajira takribani milioni 1.5, za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
"Janga la UVIKO limeathiri kiasi kikubwa sekta ya Utalii duniani zikiwemo nchi ambazo ni masoko makuu ya Utalii duniani. Kwa upande wa hapa kwetu Tanzania, idadi ya Watalii waliotembelea nchini ilipungua kutoka 1,527,230 mwaka 2019, hadi 620,867 mwaka 2020 sawa na upungufu wa asilimia 59.3, Aidha, mapato yatokanayo na Utalii yalipungua kutoka Dola za Marekani Bilioni 2.6 mwaka 2019 hadi Dola za Marekani Bilioni 0.715 mwaka 2020 sawa na upungufu wa asilimia 72.5.
"Kwa hali hii sekta ya Utalii imeanza kuimarika kunatokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali yetu. Tunampongeza sana Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuanzisha na kutekeleza mpango wa Kitaifa wa kukabiliana na janga la UVIKO19,
Hii ni utekelezaji mpango wa chanjo Kitaifa ya UVIKO19, ambao umeleta taswira mpya katika sekta ya Utalii ambapo Tanzania imekuwa eneo salama zaidi kutembelewa na watalii." Alisema Naibu Waziri Mhe. Mary Massanja.
Na kuongeza kuwa, kutokana na ushawishi huo wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imepokea fedha za Shirika la Fedha Duniani [IMF], kwa ajili ya kukabiliana na athari zitokanazo na UVIKO19.
"Sehemu ya fedha hizo, zimeelekezwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kutumika katika kuinua sekta ya utalii nchini ikiwemo utoaji wa mafunzo ya kukabiliana na janga la UVIKO 19 ambayo nimeyazindua rasmi leo Januari 29,2022, kama inavyosisitizwa na Shirika la Utalii Duniani.
Akielezea Mafunzo hayo aliyoyazindua rasmi, alisema;
"Mafunzo haya ambayo nimeyazindua leo, yatatolewa katika mikoa 26 nchini kote na yamelenga kuwafikia watoa huduma wa sekta ya Utalii takribani 3,900.
Ni wazi kwamba utalii ni sekta mtambuka, na hivyo mnyororo wake wa huduma [Toursm value/supply chain], unahusisha wadau wengi kwa kuzingatia hali hii ya mafunzo yatahusisha watoa huduma mbalimbali wakiwemo;
Watoa huduma katika tasnia ya ukarimu, malazi na chakula kama ikiwemo Hoteli, Loji na kambi za kitalii na wengine wengi." alisema Naibu Waziri, Mary Massanja.
Na kuongeza;
"Wakati wa mafunzo haya, mtapata elimu kuhusu chanjo ya UVIKO 19 na pia kupata fursa ya kupatiwa chanjo kwa wale waliotayari kupatiwa chanjo hiyo." Alisema Naibu Waziri Mary Massanja.
Ambapo aliongeza kuwa, juhudi za pamoja ziliwezesha, Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache Barani Afrika zilizokidhi vigezo kupata hadhi ya kutumia muhuri unaotambulika Kimataifa na Watalii unaotolewa wa Baraza la Usafiri na utalii Duniani [World Travel and Tourism Council- WTTC], ujulikanao kama "World Safe Travel".
Aidha, ametoa wito kwa watoa huduma za Utalii nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mafunzo hayo ambayo yatawafikia katika mikoa waliyopo.
"Wale ambao mtapata kushiriki mkawe mabalozi wetu katika kukabiliana na janga la UVIKO19 katika sekta ya utalii kwa kuwapatia ujuzi na maarifa watoa huduma wengine katika maeneo yenu ya kazi.
Wizara ya Maliasili na Utalii iliidhinishiwa kiasi cha Shilingi Bilioni 90.2 ambayo ni sawa na asilimia 6.9 ya fedha yote iliyotengwa kutekeleza majukumu mbalimbali ndani ya mwaka wa fedha 2021/2022.
0 Comments