Na Fatma Ally MDTV Dar es Salaam.
Chama Cha Alliance For Democratic Change (ADC) leo kimemtangaza rasmi Maimuna Said Kassim kuwa Mgombea wa Uspika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambae atakwenda kuchuana na wagombea wa vyama vyengine.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Hamad Rashid amesema chama chao kimempitisha mgombea huyo baada ya kamati tendaji ya Chama hicho kujiridhisha kuwa anauwezo wa kuliongoza bunge la Jamuhuri ya Muungano wa.
"Chama chetu kimempa baraka zetu zote mgombea wetu Maimuna kwani ana uwezo mkubwa na elimu ya kutoshaz pia ana weledi mkubwa hivyo anaweza kuwaongoza wabunge kama kiongozi Mkuu wa mhimili huo"amesema Mwenyekiti Hamadi
Aidha, amewataka wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumchagua mgombea huyo bila kujali itikadi ya vyama vyengine, Ili kupunguza migongano ya kihimili ndani ya nchi.
"Hatuna mashaka hata kidogo na uwezo wa Maimuna Said kwani hata katika uchaguzi mkuu uliopita aligombea ubunge katika jimbo la kilindi na alipata kura elfu kumi na nane,hivyo ana uwezo wakusimamia nakuliongoza bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" amesema Mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, amempongeza Rais wa JMT Samia Suluhu kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya hasa kuwaunganisha watanzania na hata maendeleo yanaonekana katika kipindi kifupi alichohudumu hivyo wao kama ADC wataendelea kumuunga mkono.
Naye, Maimuna Said ambae ni mteule wa nafasi ya Uspika kupitia chama hicho, akizungumza mara baada yakutangazwa kuwa mgombea amesema anashukuru Chama chake kwa kumwamini na kumuona anafaa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Nilijitathimini nikaona nina uwezo,nina elimu ya kutosha na nimewahi kuwa kiongozi katika Chuo kikuu cha Dodoma,na nimesoma masuala ya kibunge hivyo nina hakika kama wabunge watanichagua nitafanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa" amesema Maimuna.
Aidha amesema anataka kulifanya bunge kuwa la kisasa kwani katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na migongano ya kimihili ambayo inapelekea kila muhimili kusema la kwake hivyo endapo watampa ridhaa atahakikisha anakwenda kuunganisha na kufanya bunge kuwa imara zaidi.
Maimuna ameongeza kuwa anaimani kubwa atakwenda kupata kura za ndio na watanzania wategemee mabadiliko makubwa yanakwenda kutokea katika kipindi changu cha uongozi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Doyo Hassan Doyo amesema chama cha ADC hakipeleki mgombea kwa kutafuta CV kama inavyozungumzwa huko nje, bali wanawapeleka kwa ajili ya uongozi kutokana na Chama hicho kuwaanda vizuri kwa ajili ya uongozi.
Ameongeza kuwa, chama hicho moja ya kazi yake ni kuwandaa viongozi wao, ambapo tayari wana kiongozi ndani ya Serikali ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga na sasa wanakwenda kutoa kiongozi mwingine ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
0 Comments