Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na Save the Children, wakutana na wadau mbalimbali wa Haki za Binadamu kujadili ripoti ya Kikao cha Tatu cha Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) kwa mwaka 2021, hii leo Desemba 07, 2021, jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika Kikao kazi hiki ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, ambae amefungua rasmi kikao cha kujadili ripoti ya tatu ya mapitio ya hali ya Haki za Binadamu (UPR) kwa mwaka 2021.
Akimkaribisha mgeni Rasmi, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Onesmo Olengurumwa, amesema Mtandao umekuwa ukiratibu ufuatiliaji na tathmini ya Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) kwa niaba ya Watetezi wa Haki za Binadamu zaidi ya 200 Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Amon Mpanju, amewahakikishia wanachama wote wa Mtandao, pamoja na wadau wa Haki za Binadamu kuwa,maoni yote yaliyowasilishwa serikalini yatafanyiwa kazi kwa mujibu Katiba, Mila na desturi, na pia kuupongeza Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, na Asasi zingine za Kiraia, kwa kuwa karibu na serikali na kutoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa haki kwa makundi yote ya binadamu nchini.
Katika kikao hicho cha siku moja, mashirika mengine yaliyoshiriki katika uandaaji, yamewakilishwa na Ndugu Raymond Kanegene (LHRC) pamoja na Ndg. Wilbard Mchunguzi (Save the Children).
Mwaka 2021, Tanzania imefanya mapitio ya 3 ya hali ya haki za binadamu (UPR) mnamo mwezi Novemba ambapo ilipokea jumla ya mapendekezo 252 kutoka nchi mbalimbali, ambapo mapendekezo 108 tu kati ya 252 (43%) yalikubaliwa na serikali, mengine 12 (4.8%) yakiahidiwa kuzingatiwa, na mapendekezo 132 (52%) hayakukubaliwa.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mtandao, kiwango cha kukubalika kwa Mapendekezo yanayotolewa na nchi wanachama juu ya sheria mbalimbali zinazokiuka Haki za Binadamu, kinazidi kupungua kwa serikali ya Tanzania, kutoka 70% (2011), 58%( 2016) hadi kufikia 43% mwaka huu, 2021.
0 Comments