Suala la elimu bure kwa taifa letu kwa hakika wapo Watanzania kadhaa ambao wanakumbuka namna walivyonufaika na elimu bure, kabla ya uhuru na baada ya uhuru. Elimu bure hiyo iliweza kuwasaidia mno Watanzania wengi masikini kuweza kusoma......Na ADELADIUS MAKWEGA_ DODOMA.
Kwa mfano shule ya nyingi za msingi wakati wa Ujamaa zilikuwa na maktaba za vitabu ambapo maktaba hizo zilikuwa na vitabu vya kila aina na kila mwanafunzi akitakiwa kujenga utaratibu wa kuingia maktaba na kusoma. Huku walimu wa shule hizo wakifuatilia wanafunzi ambao hawajaingia maktaba kusoma.Maktaba hzio katika baadahi ya vijiji viliweza kuwa na maktaba zao.
Hapa hapa shuleni kulikuwa na stoo ya kuhifadhiwa vifaa vya elimu bure yakiwama madaftari, peni kalamu za risasi. Kila mwanafunzi aliyemaliza vifaa hivyo alifika stoo mathalani wale waliomaliza kalamu za risasi walienda na kishungi cha penseli hizo zilizokwisha. Akithibitisha kweli imekwisha hapo mtunzaji wa stoo ambaye alikuwa mwanafunzi/mwalimu alinakili jina la mwanafunzi huyo katika daftari maalumu na kumpa mpya.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa peni na madaftari ambayo yenyewe yalikaguliwa kama yamejaa na mwalimu/mwanafunzi alichana kidogo na kumwambia mtunza stoo kumpatia mwanafunzi huyo daftari jipya huku shule zingine zikiwagawia hadi mikebe.
Kwa shule za sekondari za kutwa mathalani za umma mfano Tambaza sekondari miaka 1990 ilikuwa na wanafunzi wa kidato kimoja 480 kwa mikondo 12 kwa kidato cha kwanza pekee, hivyo hivyo kidato cha pili, tatu hadi cha nne. Shule hii ilikuwa ikitoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wanaoingia shuleni mchana ambapo waliweza kula wali nyama / maharage na huku wale waliokuwa wakiingia asubuhi wakipatiwa skonzi na chai ya rangi na ndizi moja.
Hapo unaweza kutambua kuwa shule hii ilikuwa na wanafunzi 1120 hapo bado wale wa kidato cha tano na sita jumla ni karibu wanafunzi 1300. Wote hao walipatiwa chakula cha asubuhi na mchana huku kidato cha tano na sita wakipatiwa milo yote kwa kuwa walikuwa bwenini.
Jambo hilo lilikuwa ni la kawaida sana kwa shule za kutwa kwa Dar es Salaam kama vile Azania, Kisutu, Forodhani,Jangwani na hata Zanaki. Nakumbuka kuna wakati nikiwa mwanafunzi wa Tambaza tuliwahi kwenda kuwatembelea rafiki zangu waliokuwa wanasoma Forodhani na nilipofika hapo niliweza kula chakula cha mchana na kilikuwapo cha kutosha hata kwa wanafunzi wageni.
Kwa mujibu wa waraka Nambari 3, 2016 wa elimu bila malipo katika sehemu ya 3.10 .III kwa Wazazi/walezi unapiga mbiu ya mgambo juu ya,
“Wazazi na walezi kushirikiana na uongozi wa shule kuweka utaratibu wa kutoa chakula cha mchana kwa shule za kutwa na zenye Hosteli kulingana na mazingira yao. Makubaliano yao yawasilishwe kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa ajli ya kupata kibali.”
Sawa wazazi wenyewe waamue juu ya chakula cha mchana cha watoto wao alafu wakaombe kibali juu ya chakula cha mchana. Swali ni jee huyu Mkurugenzi anayeombwa kibali yeye hatambui umuhimu wa chakula cha mchana kwa wanafunzi? Je serikali kuu haitambui umuhimu wa chakula cha mchana kwa mwanafunzi ? Kwanini chakula cha mchana cha mtoto wetu wenyewe kibali kiombwe? Kwani Bodi/Kamati isiamue na chakula hicho kuanza kupikwa na kuliwa tu. Nadhania hili ni jambo la msingi na si la kujadiliwa nadhani hilo linasaidia kuongeza ufaulu wa watoto wetu shuleni.
Katika baadhi ya mikoa mathalani Songwe Wilaya ya Mbozi wazazi kila mavuno katika baadhi ya shule walijiwekea mchango wa debe la mahindi na kilo mbili za maharage ambazo hizo zinasaidia wanafunzi kula chakula cha mwaka mzima. Huku katika baadhi ya shule walilima viazi lishe ambavyo vilitumika kama chakula cha kubadilisha kwa wanafunzi
Kwa shule kama hizi za Mbozi wanazochangia chakula huwa kunakuwa na changamoto ya mpikaji, kuni, chumvi, vyombo vya kupikia na mafuta ya kupikia. Hapa Bodi/kamati za shule hujiongeza zaidi wengine huwa wanalipia pesa kidogo kwa ajili ya chumvi lakini pia nilishuhudia shule moja Wilayani Lushoto katika Jimbo la Mlalo Mwamboa ambapo wazazi walipeana zamu ya kuwapikia watoto wao wenyewe. Mwalimu akiwa bize na kusomesha tu, kila siku akina baba watatu na akina mama watatu wanaenda shuleni na kuwapikia watoto wao kwa zamu, wazazi/walezi hawa walikuwa na zamu ya mwaka mzima.
Wilaya ya Mbozi walienda mbali zaidi ambapo kila shule walikubaliana kulima viazi lishe na walilima viazi hivyo angalau ekari mbili na ekari moja ya karanga ambazo zilisaidi kuwapa wanafunzi chakula cha mchana chenye virutubisho, karanga hizo zikiwa pia kiungo cha kande na mboga.
Hawa Wanyia(Mbozi) walienda mbali mno kwa kupanda miparachichi kila shule ambayo walikubaliana kuwa yangewasaidia kuwapa kama virutubisho wanafunzi shuleni lakini pia kuwa mradi wa kuiingizia shule pesa. Nadhani hata kama miparachichi hiyo kama imekufa naamini itakuwepo kwa wale waliotilia maanani kilimo hicho na sasa wanakula matunda hayo.
Kwa hiyo shule ina mahindi, ina maharage, ina karanga ina viazi lishe na parachichi kwa hakika hata maudhurio shuleni yatakuwa maradufu, akili za wanafunzi zitakuwa imara na uelewa mkubwa na watafanya vizuri kwenye masomo pia.
Katika upande wa afya shuleni, shule zote hizi wakati wa ujama zilikuwa na wauguzi wa kutoa huduma ya kwanza ambao walikuwa wakiishi hapo hapo shuleni kutoa huduma ya kwanza pale linapotokea tatizo lolote la dharura. Wakati wale waliokuwa wakisoma shule za bweni hali ilikuwa nzuri zaidi huku wakipatiwa hadi nauli za kwenda na kurudi nyumbani na huku gharama zote zilikuwa za serikali. Hapa mwanafunzi kazi yake ilikuwa ni kusoma tu. Wengine wanatoa ushahidi katika hili wakisema kuwa baadhi ya shule wanafunzi hao walipatiwa hadi sare.
Elimu hii haikuishia katika shule za sekondari tu hadi vyuo na vyuo vikuu na ndiyo maana kama utatembelea taasisi nyingi zinazotoa mafunzo kwa ngazi ya Cheti, Diploma na hata shahada utakutana na mabwalo makubwa ya kutolea chakula kwa wanachuo. Mabwalo haya yalikuwa yakitoa huduma hiyo kwa wanachuo wanaosoma kwa gharama za serikali.
Kwa leo naweka kalamu yangu chini hapa nakutakia siku njema nikiendelea kutazama waraka nambari 3 wa mwaka 2016 wa elimu bure huku bado napigia chapuo la elimu ya ziada.
makwadeladius@gmail.com
0717649257.
0 Comments