Header Ads Widget

WANAWAKE ACT WATAKA WAZIRI NDALICHAKO AJIUZULU

 

Mwenyekiti  wa Kikosi Kazi cha Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo Taifa Pavu Juma Abdallah

Dar es Salaam:Ngome ya Wanawake wa Chama cha ACT Wazalendo imemtaka Waziri wa Elimu, Sayansi na Elimu ya Juu, Profesa Joyce Ndalichako kujiuzulu wadhifa wake kutokana na kuliyumbisha Taifa kuhusu kuendelea na masomo kwa wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito wakingali shuleni.


 Taarifa ya Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Ngome ya Wanawake Taifa, Pavu Juma Abdallah kwa vyombo vya habari leo Novemba 26,2021 imesema 

Profesa Ndalichako akiwa waziri mwenye dhamana katika Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais John Pombe Magufuli (marehemu) alishiriki kufuta haki ya watoto wa kike waliopata ujauzito wangali shuleni kurudi shuleni katika mfumo rasmi wa elimu.


Pavu amesema hatua hiyo ilikuwa ni kinyume na misingi ya haki za binadamu, mikataba ya kimataifa kuhusu haki za watoto, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za nchi.


Hatua hiuo pia ni kinyumbe na Sera ya Taifa ya Elimu, na si tu na matakwa ya Ilani ya ACT Wazalendo ya mwaka 2020 bali pia kinyume na matakwa ya Ilani ya chama tawala CCM.


"Hatua hii ya ajabu na isiyokubalika ilifikiwa kwa matamko ya hadharani yaliyotolewa na viongozi wa Serikali wakiongozwa na Rais mwenyewe hayati John Pombe Magufuli kwa madai kwamba Serikali yake haiwezi kusomesha 'wazazi'


"Chama chetu, kupitia kwa Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe kilipinga na kuchukua msimamo na hatua kali dhidi ya maamuzi yale ya Serikali ya kuwanyima watoto elimu kwa sababu ya ujauzito. Wadau wengineo pia walijitokeza na kupaza sauti zao, kukosoa na kupinga msimamo na maamuzi ya Rais Magufuli na Serikali yake."ilisema taarifa hiyo ya Pavu.


Aidha kiongozi huyo wa Ngome ya Wanawake Taifa amesema licha ya hatua hiyo, Zitto alishiriki mapambano hayo ya kutetea haki ya watoto wa kike kwa kuchukua hatua za kipekee na za kijasiri, jambo ambalo lilimletea shida kubwa ikiwemo kutishiwa hadharani kuuawa.


Alisema pia kwamba Zitto alishambuliwa, kukashifiwa na kukosewa adabu ndani ya Bunge na wabunge wa CCM hasa baada ya kiongozi huyo kuwa amechukua jukumu la kuishawishi Bodi ya Benki ya Dunia (WB) kutoipa Serikali ya Rais Magufuli mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 500 (sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 1.1 za Kitanzanai) uliolenga kwenda kuboresha mfumo na miundombinu ya elimu. 


"Zitto aliikumbusha Bodi ya Benki ya Dunia inayotoa idhini kutolewa kwa mkopo huo kuwa mkopo huo utakuja kutumika kwa ubaguzi kwa kuwaacha nje watoto wengine kwa kisingizio kuwa wamepata ujauzito wangali shuleni na hivyo hautaweza kufikia lengo lililokusudiwa la kuwakomboa watoto wa Kitanzania kielimu.


"Zitto alieleza kuwa hatua ya serikali ya kuwaondoa kwenye mfumo rasmi wa elimu watoto waliopata ujauzito na kuwapeleka katika mfumo usio rasmi ambako wangeenda kujifunza ususi, ufuaji nguo, upishi na stadi nyinginezo kama hizo, haifai kwani inaangamiza ndoto, vipaji na matarajio ya watoto hao. Alifafanua kuwa mimba kwa mtoto haipaswi kuwa adhabu ya kumnyima elimu anayohitaji yeye mwenyewe. Zaidi, kumnyima mtoto wa kike elimu anayostahiki ni kurudisha nyuma jitihada za ukombozi kwa waanawake kwani kuna uzoefu na mifano mingi ya wanawake ambao walipata ajali ya ujauzito wangali shuleni na walipopewa nafasi ya kurejea shule na kuendelea na masomo yao, walifanya vizuri na kuwa viongozi na wataalamu mahiri na wenye kutumainiwa kwenye fani mbalimbali.


"Bodi ya Benki ya Dunia ilikubaliana na hoja zilizotolewa na Kiongozi wetu Ndg. Zitto na hivyo kusitisha utoaji wa mkopo huo hadi pale Serikali itakapoachana na msimamo wake wa kuwabagua watoto waliopata ujauzito katika mfumo rasmi wa elimu.


Juzi Novemba 24, 2021 Serikali kupitia kwa Waziri wa Elimu Joyce Ndalichako ilitangaza kuachana na msimamo wao wa awali wa kuwatupa nje ya mfumo rasmi watoto waliopata ujauzito na kurejea kwenye sera, sheria na misingi ya haki za watoto kupata elimu kwa kutangaza rasmi kuwa sasa watoto wa kike waliopata ujauzito wangali shuleni, wataendelea na masomo yao katika mfumo rasmi wa elimu mara baada ya kujifungua.


Pavu aliendelea kuwataka watu wote waliomtukana, kumkashifu na hata kumwombea kifo  Zitto, wajitokeze na wamuombe radhi hadharani ma kufanya hivyo si jambo la fedheha, bali ni kuonesha ujasiri wa kukiri makosa na kuonesha uungwana. 


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI