Kwa wakati huo nilikuwa mwanafunzi wa shule ya Sekondari Tambaza na shule za sekondari zote zisizo za bweni yaani za kutwa kwa jiji la Dar es Salaam zilikuwa chache mno nakumbuka kwa mwaka 1989 na 1990 jumla ya wanafunzi waliokuwa wakifaulu kutoka darasa la saba kwenda sekondari walikuwa hawazidi 5000, yaani kila mwaka walikuwa hawazidi 2500........NA ADELADIUS MAKWEGA _DODOMA.
Hiyo ilikuwa idadi ndogo sana kwa hiyo shule za sekondari zote za serikali zilikuwa katikati ya jiji hili. Kwa hiyo kwenda sekondari ilikuwa ni kwenda kuwa mjanja zaidi maana sasa ilikuwa unatoka shule za vichochoroni kwenda kusoma shule za Forodhani (Watoto wa kishua), Tambaza (Gangwe), Azania (John Kisomo), Kisutu (sister duu), Jangwani, (sister duu) , Zanaki (sister duu) na hata Kibasila japokuwa yenyewe ilikuwa shule pekee ya sekondari ya umma iliyokuwepo Wilaya ya Temeke.
Kwa muda wa jioni, kama umerudi nyumbani kutoka shuleni tulitumia kushinda katika shule za msingi ambazo tulisoma au shule zilizo jirani na maeneo yetu ya nyumbani. Nafasi hiyo tuliweza kukutana na kaka na dada zetu walio madarasa ya juu yaani kidato cha II, III, na IV huku wakitufundisha masomo mbalimbali na muda mwingine ulikuwa wakati wa kupiga soga pia.
Kama ilivyokuwa desturi yangu ya kwenda shule na jioni kwenda kujisomea shule ya msingi jirani, siku moja nilienda shule ya msingi Mbagala kujisomea, nilifika hapo nilikutana na rafiki zangu kadhaa ambao tulikuwa tukijisomea pamoja na baada ya kumaliza kujisomea huko tulikuwa tunatoka nje kutazama mazoezi ya mpira wa miguu kwa timu ya ABUJA FC (Kizuiani), TESEMA FC (Mbagala 77) na AGATON FC (Mangaya) zote hizo zilikuwa timu za Mbagala kutoka maeneo hayo kwa wakati huo.
Unapokuwa unasoma katika madarasa haya kwa kuwa mimi ni mwanafunzi wa sekondari huwa pana wanafunzi wa shule za msingi hasa wale wa darasa la saba wanaojiandaa na mitihani yao na wao hujijengea utaratibu wa kusoma kwa hiyo mara nyingi wanakuwepo madarasani wakijisomea pia au wakikuona utasikia kaka tusaidie hesabu hii na ile basi hapo unakuwa mwalimu wa wao kila siku wanakuja kwako..
Hili kuepusha kusumbuliwa sana na wanafunzi hawa basi huwa mara nyingi ninakaa dawati la mwisho kabisa na kwenye kona, wenyewe enzi zetu tulikuwa tunasema unakaa nyuzi 90. Katika kona hiyo ya nyuzi tisini darasani ukiingia mkono wa kushoto kama mtu akiingia kwa haraka bila ya kutazama kwa kina hatoona kitu. Au pengine mtu akitoka nje na kuigia darasani akiwa amepigwa na jua machoni kwa muda mrefu anaweza kuingia akafanya kituko chake, wala hawezi kutambua kuwa darasani humo kuna mtu.
Basi nilikaa humo darasani nikiwa najisomea taratibu na sikuwa na ili wala lile. Gafla nikasikia hatua za watu ko ko ko ko… mara nikasikia tii mizigo ikishushwa, nikiwa nimeyatoa macho yangu niliona wanaingia katika darasa hilo watu kadhaa wenye mizigo na mtu mwingine akisema wekeni mizigo yenu hapahapa.
Kweli mizigo hiyo ikatuliwa chini katika mlango pembeni ili mtu akipita kwa nje asiwaone kama kuna watu darasa. Wakaambiwa chuchumaeni, kweli ndugu hawa walikuwa watiifu sana walifanya hivyo. Mimi nilipoziona hizo harakati nilijua hapa pana jambo si bure, nilishituka lakini nikawa kimya kabisa.
“Haya hapa kila mmoja anatakiwa kutoa hamsini hamsini, maana nyinyi mmezidi sana kila siku na tumewaambia muwache haya mambo yenu lakini bado.”
Alisema mtu mmoja ambaye sikuweza kumuona vizuri lakini mwili wake ulikuwa nusu ndani ya darasa na nusu nje ya darasa. Basi wale ndugu waliokuwa wamechuchumaa walichangishana kimya kimya huku pesa zingine zikianguka chini. Hapo darasani palikuwa kimya bali kwa mbali zilisikika sauti za ndege aina ya sholwe ambao wanapenda kujenga katika majengo za serikali tu.
Niliendelea kutazama sinema hiyo ya bure nikawaona watu kadhaa ambao kwa hakika wao walikuwa maarufu sana kwa kuuza gongo mtaani kwetu na mmojawapo alikuwa mama mmoja anayefahamika kama Mwarongo Chongo.
Pesa hiyo ilikusanywa vizuri kabla hawajamaliza nikawatazama vizuri jamaa hawa niliwabaini kama askari hivi. Basi wakakabidhiwa wale jamaa pesa yao na wale waliokuwa wamechuchumaa wakaruhusiwa.
“Kimbieni haraka, hakuna kugeuka nyuma na hatutaki kuwaona hapa.”
Walibaki hawa jamaa kama sita hivi mpaka muda huu hawakutambua kama mle darasani mimi nipo nikifuatilia ile sinema ya bure. Jamaa hawa kwa kuwatazama nilihisi kuwa wanatokea Kituo cha Polisi Mbagala Maturubai na namna walivyokuwa wakiongea na kuitana majina wakitanguliza neno afande.
“Haya jamani haraka haraka, hapa kila mmoja hamsini hamsini.”
Yule mmoja ambaye nadhani alikuwa mkubwa wao alisema hivyo.
Wakati mgao huo ukiendelea kwa amani na utulivu darasani hapo na kama unavyotambua pesa uchawi wa kizungu na mie tamaa ikanijia.
“Ahhh Jamani kwanini mnagawana peke yenu? Na mimi nataka mgao huo.”
Nilisema kwa sauti ya juu, jamaa wakataka kukimbia, nikawaambia hakuna kukimbia hapa, nawajua wote hadi majumbani kwenu. Duu jamaa wakawa wapole jamaa walishituka sana huku vijasho vikiwatoka. Ehh humu ndani kumbe kuna mtu, wewe bwana mdogo vipi?(jamaa wakawa wansema). Nikawafuata walipo kwa kupanda juu ya madawati ya shule hii ya msingi. Sasa walishatambua kuwa yote waliyoyafanya nimeyaoni na mimi ni mwenyeji pale nadhani kuliko wao. Maana uwanjani wako makaka wakubwa wengi kama akina Mwinjuma Kondo na Akina Linje wakicheza mpira. Wasingekubali mdogo wao nionewe.
Saikolojia ya binadmu ni kuwa anapofanya jambo lake baya akiwa anajua kuwa hakuna mtu anayemuona anakuwa na amani sana lakini jamaa hawa walikosa amani na kujiamini kabisa kwa kuwa kila kitu nilikishuhudia. Looo basi mmojawapo nadhani alikuwa mkubwa akawaambia mpeni dogo shilingi 25. Jamaa wakasalimu amri, Ilikusanywa pesa hiyo harakaharaka nikakabidhiwa. Jamaa wakaenda zao.
Hiyo shilingi 25 ilikuwa nyingi sana maana nauli ya basi kwa wanafunzi ilikuwa shilingi 1 na wakubwa walikuwa wakilipa kati ya shiilingi 7-10 kwa safari ya kutoka Mbagala hadi Temeke.
Nikaweka pesa yangu mfukoni, wakati huo TAKURU wala TAKUKURU hazikuwepo, wala wazo la Jaji Joseph Warioba la kuundwa kwa chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa halijatolewa. Maana nakumbuka wazo hilo alilitoa Mzee Warioba katika Tume yake ya Rushwa ya mwaka 1997 ambapo alipewa kazi hiyo na Rais wa Awamu ya Tatu Ndugu Benjamin Mkapa.
Nikiwa na shilingi zangu 25 mfukoni, je nibaki niendelee na masomo au niondoke? Nilijiuliza maswali mengi, je hawa jamaa wakirudi wakinibambikia kesi ya kukutwa na bangi nitapona? Maana uwongo wa Askari si Ukweli wa Raia. Nikafungasha madaftari yangu, nikatoka nje na kutazama mazoezi ya mpira kiwanjani na kurudi zangu nyumbani.
makwadeladius@gmail.com
0717649257





0 Comments