Header Ads Widget

POLISI ROMBO WADAIWA KUMVUNJA RAIA MGUU KWA SHOKA,AJERUHIWA BEGA NA MBAVU TATU ZA KUSHOTO ZAHAMA....

Katika tukio lisilo la kawaida mkazi wa kitongoji cha Lokoro kijiji cha Kikelelwa  katika kata ya Motamburu Tarakea Aniceth Thadey Kimario(35) amedai kujeruhiwa vibaya na askari wa kituo cha polisi Tarakea kwa kumshambulia na shoka la kuchongea mawe na kusababisha  kuvunjika mguu wa kulia, bega la kushoto kujeruhiwa pamoja na mbavu tatu za upande wa kushoto kuhama na majeraha mengine huku akishindwa kujua kosa lake. mwandishi wa matukio daima Gift Mongi anaripoti kutokea Rombo

Akizungumza  akiwa katika wodi ya Mtakatifu Fransis kitanda namba 13 katika hospitali ya Huruma anapoendelea kupatiwa matibabu Acineth alisema ilikuwa majira ya saa 11.07 za jioni octoba 29 akitokea kazini kwake katika kiwanda cha Chipoli na ndipo akakuta ugomvi uliowahusisha walimu wa sekondari Motamburu pamoja na shemeji yake anayefahamika kwa jina la Gedson Steven.

HALI ILIVYOKUWA

Alisema baada ya kuukuta ugomvi huo alilazimika kuingilia kati na kuwaachanisha ambapo kila mtu aliendelea na mambo yake na yeye akasogea duka la jirani na kuagiza kinywaji huku akimsubiria bosi wake ili aweze kulipwa ujira wake kwani malipo hufanywa kila ijumaa jioni.

Anasema wakati akiwa anaendelea kupata kinywaji ghafla ikatokea gari la polisi wakiwemo askari wanne na mwalimu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Katembo miongoni mwa wale waliokuwa na ugomvi na ndugu yake na kuamriwa  kupanda kwenye gari ya polisi huku akiwa hana hili wala lile pamoja na yule shemeji yake.

Kwa mujibu wa Aniceth ni kuwa walipanda kwenye gari la polisi na yule shemeji  yake na kupelekwa kituo kidogo cha polisi Lokoro  na kuanza kupigwa huku wakielezwa kuwa hawataweza kushindana na serikali.


KWANINI SHOKA LILITUMIKA?

Acineth kwa maelezo yake alidai katika mateso waliyopewa kituoni hapo silaha iliyotumika kuwajeruhi ni shoka dogo ambalo hutumika katika shughuli za kuchongea matofali.

"Wale askari kale kashoka huwa wanatembea nako kwa ajili ya kuharibia mitambo ya gongo na kutoboa madumu yenye gongo hivyo walivyokuja kutukamata walitoka kwenye operesheni zao hizo eneo la Kikelelwa juu"alisema


WAHAMISHIWA KITUO CHA POLISI TARAKEA.

Alisema baada ya kupata kipigo kutoka kwa askari hao waliwapeleka katika kituo cha polisi Tarakea huku akiwa tayari kavunjika mguu,bega la kushoto kuumia sambamba na mbavu tatu za kushoto  kuhama na walipewa fomu ya matibabu(PF3)iliyoandikwa kuwa ni ajali na kupelekwa kituo cha afya Tarakea na kutelekezwa nje wakiwa hawajitambui.

Alisema wakiwa hapo ndipo ndugu zao wakawa wanawafuatilia nyuma kujua kulikoni na ndipo wakakutwa wametelekezwa bila msaada wowote na hatimaye wakapelekwa hospitali ya Huruma kwa matibabu zaidi.


MASHUHUDA WAZUNGUMZA.

Erasamus Tarimo (32)ambaye ni dereva wa bodaboda alisema aliwashuhidia polisi hao wakiwapakiza watu wawili kwenye gari siku hiyo katika eneo la tukio na kuwapeleka kituo kidogo cha Lokoro ambapo hata hivyo hakiweza kujua chanzo chake ni nini.

"Niliwaona polisi hiyo ijumaa wakiwabeba watu wawili lakini sikuweza kujua mara moja tatizo lilikuwa ni nini hadi nilipokuja kupata taarifa baadae kuwa walienda kupigwa ila walipopakizwa walikuwa ni wazima"alisema 

Mwenyekiti wa kitongoji cha Lokoro Adolf Shayo alisema tukio hilo amelisikia limetokea katika eneo lake lakini asingeweza kulizungumzia kwa undani kwani alikuwa safarini.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kikelelwa Justin Shirima alisema kuwa hana taarifa juu ya tukio hilo hivyo apewe muda na kufuatilia  ili aweze kuujua undani wa tukio hilo kama litakuwepo ama la.

Polycarp Joseph ni kaka wa majeruhi huyo ambapo alisema kutokana na ulemavu alioupata ndugu yake shughuli za kumuingizia kipato zimesimama na kuiomba serikali kupitia mamlaka husika kuingilia kati.

"Tukiwa pale hospitali kuna askari waliokuja na kusema kuwa gharama zote za matibabu wanaenda kuchangishana watalipa kwahiyo sasa swali langu, je ndugu yangu akiruhisiwa atakula nini na mtoto aliyefaulu ataendaje shule?"alihoji

Alisema (leo) tarehe 05.11 walikuja askari katika hospitali ya Huruma na kulipa kiasi cha fedha anachodaiwa ndugu yake kama gharama za matibabu ambapo walilipa kiasi cha laki tano huku gharama zikiwa ni zaidi ya laki sita.

KAULI YA RPC KILIMANJARO.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo kwa njia ya simu kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro ACP Simon Maigwa alisema yupo nje ya ofisi kikazi na kuwa hana taarifa kuhusiana na tukio hilo na kuwa atalifuatilia.

"Nipo huku Mkomazi na kuhusu tukio hilo naona ni geni ni tofauti na nililokuwa nalifikiria ila ngoja nitalifuatilia"alisema Kamanda Maigwa

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI