Naibu Waziri wa wizara ya mifugo na uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mkuranga Mheshimiwa Abdallah Ulega amesema amewasilisha maombi ya kuwa na mkoa wa kitanesco ilikuweza kuwatosheleza mahitaji ya umeme kwa wananchi na viwanda vingi vilivyopo wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji.
Amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kata za Vikindu na Mwandege kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa yanayojengwa kwa fedha za kupunguza maambukizi na kusambaa kwa ugonjwa wa UVIKO 19 kutoka IFM jimboni kwake Mkuranga.
Alisema idadi ya wananchi wilaya ya Mkuranga hasa kata za Vikindu na Mwandege ni kubwa mno ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya wawekezaji wa viwanda vingi vilivyopo katika wilaya hiyo ni sababu tosha ya kuweza kuwa na mkoa wake wa kujitegemea katika huduma muhimu ya Ugawaji wa umeme.
Mheshimiwa Ulega alisema mahitaji ya umeme kwa sasa katika wilaya ya Mkuranga ni kubwa pia kwasababu ya ongezeko la wahamiaji wa kila siku kutoka jijini Dar es salaam na mikoa mingine.
"Kuna haja ya kuwa na mkoa wetu wa kitanesco ili itupunguzie gharama hata tukihitaji nguzo moja ya umeme kuifuata Wilaya ya Kibaha ambako ndio kuna makao ya mkoa wa TANESCO mkoa wa Pwani ni mbali huku tukiwa na idadi kubwa ya viwanda na wahitaji wakubwa wa umeme" alisema Mheshimiwa Ulega.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Khadija Nasri alisema Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji wanauhitaji mno na kwa haraka mno huo mkoa wa kitanesco iliisaidie kusogeza huduma za umeme karibu na jamii hiyo na kupunguzia gharama wananchi na wamiliki wa viwanda katika wilaya hizo.
Khadija alisema vifaa vyote vinavyohusika na usambazaji wa umeme katika wilaya zao kwa sasa vipo makao makuu ya mkoa wa Pwani Wilayani Kibaha ambako ni mbali.
"Tunapotaka kusambaza umeme inatubidi kuenda Wilaya ya kibaha ambako ni mbali hivyo inatuwia ugumu kufikisha vifaa huku katika wilaya zetu lakini tukipata mkoa wetu wa kihuduma itatusaidia mno" alisema Khadija.
"Sisi tukitaka nguzo, transfoma na vifaa vingine tukipata mkoa wetu tutapata hapa hapa Wilayani Mkuranga na tutasaidia Wilaya jirani wapate huduma kwa karibu" alisema Khadija.
"Kama unavyofahamu Kibaha ni mbali na gharama za usafirishaji kweli zinatuwia vigumu hivyo tunahitaji sana mkoa wa kitanesco maana Wilaya ya Mkuranga inaongoza kwa idadi kubwa ya viwanda Nchini ambapo kuna viwanda zaidi ya 1200" alisema Khadija.
0 Comments