MBUNGE wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda amempongeza mkuu wa Chuo Cha Maendeleo Mbinga Lothy Mwang'onda kwa kusimamia vema miradi ya ujenzi wa majengo ya chuo hicho kwa kuzingatia viwango vya ubora kama maagizo ya Serikali yanavyotaka......Na Amon Mtega, Mbinga.
Mbunda amezitoa pongezi hizo wakati wa mahafali ya 44 ya wahitimu 87 wa chuo hicho ambapo wanachuo wa fani za ufundi wa aina mbalimbali wametunukiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo.
Mbunge huyo ambaye amekuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo kabla ya kuelekea kwenye ukumbi wa sherehe za kuhitimu mafunzo hayo alipita kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa majengo ya chuo hicho na baada ya kujiridhisha ndipo alielekea kwenye ukumbi wa sherehe hizo.
Mgeni rasmi huyo amesema kuwa licha ya kufurahishwa na wahitimu wa fani mbalimbali za ufundi katika chuo hicho lakini bado amefurahishwa na usimamizi mzuri miradi wa ujenzi wa majengo mapya ya chuo hicho ambayo yamebadilisha muonekano wa chuo na kukifanya kiwe bora zaidi kupitia majengo hayo huku akiwataka majengo hayo yasiharibiwe ili kutoa fursa kwa vizazi vijavyo viweze kuyatumia.
Aidha katika hatua nyingine mbunge huyo baada ya kupokea risala toka kwa wahitimu pamoja na tarifa ya mkuu wa chuo amesema kuwa changamoto zote ikiwemo ya maji amesikia na kuwa kuna mradi mkubwa wa maji kwenye Jimbo hilo ambapo maji yake yatasambazwa eneo kubwa la mji wa Mbinga pamoja na chuoni hapo.
Hata hivyo kabla ya kuwatunuku vyeti wahitimu hao Mbunge huyo amewataka wakienda ulayani wakaitumie vema elimu ya ufundi waliyosomea ili kuendana sambamba na mpango wa Serikali ya awamu ya sita inayoongonzwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mmoja anatumia fursa aliyonayo ikiwemo ya ufundi.
Pia Mbunge Mbunda amewataka wakazi wa Jimbo hilo kukitumia kikamilifu chuo hicho kwa kuwapeleka vijana wao ili mwisho wa siku vijana hao waweze kujiajiri au kuajiriwa kulingana na fani wanazokuwa wamezisomea.
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Lothy Mwang'onda awali amesema kuwa licha ya kuwepo kwa mafanikio ya miradi ya ujenzi wa majengo hayo mapya changamoto ipo kwa idadi ya watumishi kuwa ni wachache jambo ambalo linaweza kusababisha baadhi ya mambo kuchelewa kutekelezeka kwa wakati.
Mkuu huyo amesema kuwa licha ya changamoto ya watumishi lakini chuo kimejipanga vema na kuwa amewataka wazazi kuwapeleka vijana wao kwenda kupatiwa mafunzo kwenye chuo hicho kwa kuwa miundombinu ipo bora ikiwemo na chakula.
Nao baadhi ya wahitimu hao Monika Mhagama na Elizabeth Chedego ambao wamechukua fani ya Ushonaji nguo wamesema kuwa ufundi huo wataenda kuutumia vema ili kuhamasisha kwa baadhi ya vijana ambao hawajabahatika kupatiwa mafunzo hayo kutumia fursa ya kwenda kusomea ufundi huo.
Katika mahafali hayo yamehudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Diwani wa kata ya Losonga Magreth Ngongi ambaye ametoa msaada wa vifaa vya kufanyia mitihani kwa wahitimu hao 87 .
0 Comments