Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam limesema litahakikisha wahalifu wote wanakamatwa na kufikishwa mahakamani huku likijipanga kuwadhibiti majambazi wanaotumia silaha isivyo halali. mwandishi wa matukio daima Fatma Ally anaripoti kutokea Dar Es Salaam
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Mkoa wa Dar es salaam ACP Muliro Jumanne Muliro alisema jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa 8 kwa uhalifu wa unyang’anyi kwa kutumia silaha maeneo ya Kimara.
Alisema kuwa, watuhumiwa hao walikuwa wanajaribu kunyang’anya gari aina IST na huku wakiwa na silaha lakini kikosi cha polisi kilifanya jitihada zake kupambana na wahalifu hao kisha kuwakamata.
"Kikosi maalumu cha polisi Novemba 14 mwaka huu wakati wakiwa katika majukumu yao maeneo ya kimara walijibizana na watuhumiwa hao kwa kutumia risasi kisha kumjeruhi jambazi mmoja ambaye alikimbizwa hospitali kupatiwa huduma lakini alipoteza maisha" alisema kamanda ACP Muliro.
Katika tukio lingine, jeshi la polisi linawashikilia wahalifu wengine 6 wanaonyang’anya kwa kutumia nguvu ambapo wamekiri kufanya matukio hayo Mkoani Pwani na Dar es salaam ambapo waliiba dola 2000, saa, lap top na simu.
"Dhumuni letu kama Jeshi la Polisi siyo kuuwa wahalifu ila tunajitahidi kuhakikisha kunusuru uhai wao ili kupata ushahidi ila pale wenyewe wanapojaribu kuwarushia askari wetu nasi tunajihami wakirusha moja tunarusha tatu “alisema Kamanda ACP Muliro
Aidha Kamanda Muliro alisema jeshi la polisi linatekeleza kazi zao kwa kuzingatia sheria na halipo kwa ajili ya kumuonea mtu.





0 Comments