Header Ads Widget

VIONGOZI SUDAN WAKAMATWA, HUKU KUKIWA NA RIPOTI ZA MAPINDUZI YA KIJESHI

Watu wenye silaha wamewakamata baadhi ya maafisa wa serikali ya mpito ya Sudan majumbani kwao, taarifa zikisema kuwa mzozo wa kisiasa unazidi kuongezeka.

Mawaziri wanne wanashikiliwa na wanajeshi ambao hawajafahamika muda mfupi kabla ya alfajiri ya Jumatatu huku ripoti moja ikisema Waziri Mkuu Abdallah Hamdok pia amekamatwa lakini bado haijathibitishwa.

Hata hivyo haijafahamika bado ni kina nani hasa wanaotekeleza ukamataji huo huku Jeshi la nchi hiyo halijasema lolote mpaka sasa hata hivyo vyombo vya habari vinasema kwamba wanajeshi wasiotambulika wameizingira nyumba ya waziri mkuu Abdalla Hamdok .

Runinga ya Al Hadath inaripoti kwamba wanajeshi wamewakamata mawaziri wanne na mwanachama mmoja wa serikali ya mpito kulingana na vyanzo ambavyo havijatambuliwa.

Reuters pia imeripoti kwamba wanajeshi walivamia nyumba ya mshauri wa masuala ya habari wa waziri mkuu na kumkamata mapema Jumatatu.

Muungano wa Wataalamu nchini humo umewataka raia kuingia barabarani ili kufanya maandamano kwa lengo la kuzuia mapinduzi hayo ya kijeshi. Kundi la watu wanaounga mkono demokrasia pia, wametoa wito wa wafuasi wao na wanaounga mkono demokrasia kutokubali mapinduzi yoyote ya kijeshi.


Hatua hiyo inajiri huku kukiwa na ripoti kuhusu kuzimwa kwa huduma ya mtandao nchini humo.

Mashuhuda wanasema mitandao haipatikani katika mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum, wakati kukiwa na picha za watu wenye hasira zikisambaa kwenye mitandao wakionekana kuchoma matairi mtaani.

Hata hivyo Wanajeshi wamepelekwa mtaani kwenye jiji hilo, likizuia watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, mmoja wa mashuhuda aliiambia Reuters huku Uwanja wa ndege wa Khartoum sasa umefungwa, na safari za ndege za kimataifa zikihairishwa.

Chanzo; BBC Swahili

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI