Header Ads Widget

JKT LAWATAKA VIJANA KUJITOKEZA KUJIUNGA NA MAFUNZO YA KUJITOLEA 2026/27

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media, Dodoma


VIJANA wenye elimu na ujuzi katika taaluma mbalimbali nchini wametakiwa kutumia fursa ya kujiunga na Mafunzo ya Kujitolea ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mwaka 2026/27, huku nafasi zikitolewa kwa wahitimu wa vyuo vya kati, vyuo vikuu pamoja na wenye ujuzi wa fani mbalimbali za ufundi.


Wito huo umetolewa leo, Novemba 12, 2026, jijini Dodoma na Mkuu wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Nduka Mabele, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Jeshi hilo.


Amesema vijana wenye sifa wanapaswa kuwasilisha maombi yao kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanakoishi, ambazo zitasimamia zoezi la kupokea maombi na kuchagua vijana watakaopata nafasi za kujiunga na mafunzo hayo.


"Katika mwaka huu wa mafunzo, JKT limeweka msisitizo kwa vijana wenye elimu ya stashahada na shahada katika taaluma zinazohusiana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Sayansi ya Kompyuta, Mifumo ya Taarifa za Biashara pamoja na Usalama wa Mitandao, " Amesema.



Kwa upande wa wahitimu wa stashahada, taaluma zinazohitajika ni Teknolojia ya Habari, Mifumo ya Taarifa za Biashara, Sayansi ya Kompyuta, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Usalama wa Mitandao na Uchunguzi wa Kitaalamu wa Makosa ya Kidijitali.


Aidha Amesema, wahitimu wa shahada wanatakiwa kuwa na taaluma za Sayansi ya Kompyuta, Teknolojia ya Habari, Uhandisi wa Kompyuta, Teknolojia ya Habari za Biashara, Usalama wa Mitandao, Uchunguzi wa Kitaalamu wa Makosa ya Kidijitali pamoja na Uhandisi wa Mitandao ya Kompyuta na Usalama wa Taarifa.


Mbali na wahitimu wa vyuo vya kati na vyuo vikuu, nafasi hizo zimetolewa pia kwa vijana wenye taaluma za ufundi na ujuzi wa vitendo katika fani mbalimbali zikiwemo uchomeleaji, ufundi magari, umeme, ufundi bomba, ufundi rangi, uashi na TEHAMA.


Fani nyingine zinazotajwa ni ubunifu wa mavazi, ukarani, useremala, ushonaji, ufundi friji na vyozovi, hivyo kutoa nafasi kwa vijana wenye ujuzi wa vitendo katika maeneo mbalimbali kutumia fursa hiyo kujiunga na mafunzo ya JKT.


"Usaili wa vijana watakaoomba kujiunga na mafunzo hayo unatarajiwa kuanza Novemba 16, 2026, katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, " Amesema Mkuu huyo


Vijana watakaofaulu usaili na kuchaguliwa wanatakiwa kuripoti katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa kuanzia Desemba 10 hadi 15, 2026, kwa ajili ya kuanza mafunzo hayo.



Mkuu huyo wa Utawala JKT amefafanua kuwa vijana watakaopata nafasi hizo hawapaswi kuchukulia mafunzo hayo kama njia ya kupata ajira pekee, bali wanapaswa kuyaona kama fursa ya kujijengea nidhamu, uwezo na ujuzi utakaowawezesha kujitegemea kiuchumi baada ya kukamilisha mkataba wao wa kulitumikia Jeshi hilo.


Aidha, mafunzo hayo yanalenga kuwaandaa vijana kutumia maarifa na ujuzi watakaoupata katika shughuli mbalimbali za uzalishaji, kujiajiri na kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazowapatia kipato, kujiletea maendeleo yao binafsi na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI