Header Ads Widget

URUSI YAMWACHIA HURU RAIA WA MAREKANI STEPHEN HUBBARD

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Urusi imekubali kumwachilia raia wa Marekani aliyefungwa jela kwa tuhuma za kupigana upande wa Ukraine, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.

Putin amesema Stephen Hubbard amepelekwa katika Uwanja wa Ndege wa Pulkovo wakati wa mazungumzo yake na mjumbe wa Marekani Steve Witkoff mjini St Petersburg.

Stephen Hubbard, mwalimu wa zamani kutoka Michigan, alihukumiwa kifungo cha karibu miaka saba katika koloni la adhabu nchini Urusi mwaka 2024.

Moscow ilimtuhumu kupigana katika kikosi cha ulinzi cha Ukraine mjini Izyum kabla ya kukamatwa na majeshi ya Urusi.

Marekani ilikuwa imemtaja kama aliyekuwa amezuiliwa isivyo halali, huku Rais Donald Trump akisema aliwasilisha suala lake kwa Vladimir Putin.

"Mtaona kitakachotokea," Trump aliwaambia waandishi wa habari. "Tumekuwa tukifuatilia suala la Hubbard."

CBS News, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani, iliripoti kuwa Hubbard alikuwa na matatizo ya afya na alitarajiwa kusafirishwa hadi jimbo la Texas kwa ajili ya matibabu.

BBC imewasiliana na Ikulu ya White House kuomba maoni kuhusu suala hilo.

Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi viliripoti kuwa Witkoff alimshukuru Putin kwa kuachiliwa kwa Hubbard na pia, kwa niaba ya Trump, kwa makubaliano yaliyofikiwa na Washington mapema mwezi huu ya kuagiza dizeli kutoka Urusi.

Putin alisema wakati wa mkutano huo kwamba shehena ya kwanza ya dizeli chini ya makubaliano hayo itaondoka Urusi ndani ya siku mbili hadi tatu zijazo, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la TASS.

Makubaliano hayo ya dizeli yamemkasirisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na yameendelea kuzorotesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kyiv na Washington.

Wakati wa mkutano wa Jumatano mjini St Petersburg, Witkoff alionekana kwenye televisheni ya Urusi akisema kuwa makubaliano hayo ni mfano kwa Ukraine wa kile kinachoweza kupatikana kupitia ushirikiano.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI