Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendelea kuimarisha uwezo wa Wajumbe wa Bodi za Zabuni kutoka taasisi nunuzi nchini kupitia mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma na matumizi ya Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kielektroniki (NeST), kwa lengo la kuongeza ufanisi katika michakato ya ununuzi wa umma.
Akifungua mafunzo hayo jijini Morogoro, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt.Mussa Ali Mussa, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu wa Mkoa huo, Sebastian Masanja amewataka wajumbe hao kuzingatia uadilifu, uzalendo na weledi katika kutekeleza majukumu yao, akisisitiza kuwa matumizi sahihi ya mfumo wa NeST yanapaswa kwenda sambamba na misingi ya maadili na kutanguliza maslahi ya Taifa.
Amesema mfumo wa NeST unaimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika ununuzi wa umma, huku akieleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uwezo katika matumizi ya moduli ya Bodi za Zabuni, usimamizi wa mikataba na utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia sheria na kanuni za ununuzi wa umma.
Aidha, amewataka washiriki kutumia maarifa watakayoyapata kuboresha utendaji katika taasisi zao na kuhakikisha michakato ya ununuzi inafanyika kwa wakati, ubora na thamani halisi ya fedha za umma.
Awali Mkurugenzi wa Utafiti, Maendeleo na Ubunifu wa PPRA, Mhandisi Masunya Eliakim Nashon, amesema mamlaka hiyo inalenga kuhakikisha washiriki wa mafunzo wanafahamu matakwa ya Serikali katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Naye Meneja wa Kuendeleza Uwezo na Huduma za Ushauri wa PPRA, Gilbert Kamnde, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuhakikisha watumiaji wa mfumo wa NeST na wote wanaojihusisha na masuala ya ununuzi na ugavi wanapata elimu sahihi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Benedict Bugambi na Lenatha Miruko, wamesema mafunzo hayo yatawaongezea ujuzi na kuwasaidia kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma.









0 Comments