Header Ads Widget

TANAPA YABAINISHA: KILA MTALII ANAYEWASILI JNIA NI FURSA YA KUITANGAZA TANZANIA KIMATAIFA



Na. Jacob Kasiri - Dar es Salaam.


Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limebainisha kuwa kila mtalii anayewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa, huku madereva wa magari ya abiria na watalii wakitajwa kuwa mabalozi wa pili wa nchi kwa wageni wanaoingia nchini. 

TANAPA imesisitiza kuwa mchango wa maafisa usafirishaji hao katika sekta ya utalii haiishii tu kwenye usafirishaji wa wageni pekee, bali ni daraja la kutoa taarifa sahihi za vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini, taarifa hizo  hujenga taswira chanya kwa Taifa na kuongeza idadi ya watalii na mapato.

Akizungumza leo Oktoba 30, 2026 katika ukumbi (Terminal 3 JNIA) jijini Dar es Salaam na madereva hao,  Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Fredrick Malisa kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA alisema, “Ninyi Madereva ni miongoni mwa Watanzania wa pili baada ya Maafisa Uhamiaji kukutana na wageni wanapowasili nchini. Hivyo, namna mnavyowapokea wetu, lugha mnayotumia, nidhamu, uaminifu na ubora wa huduma mnazowapatia vina mchango mkubwa wa kujenga taswira na sifa ya Tanzania mbele ya jumuiya za kimataifa.”

Aidha, Kamishna Malisa aliwahimiza maafisa usafirishaji hao kujenga utamaduni wa kuwapokea wageni kwa tabasamu, heshima, ukarimu wa kitanzania, kujifunza kuhusu vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini kwani maarifa hayo yatawawezesha kutoa taarifa sahihi kwa wageni, kuwashauri maeneo ya kutembelea na kuwahamasisha kugundua utajiri wa vivutio vya asili, utamaduni na historia ya Tanzania.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Ofisi Kiunganishi - Dar es Salaam Neema Mollel na muandaaji wa semina hiyo alisema kuwa uhifadhi na utalii ni sekta zinazotegemeana kwa sababu maendeleo ya utalii endelevu yanategemea uhifadhi wa wanyamapori, misitu, mito na mazingira kwa ujumla. 

Kamishna Mollel aliongeza kuwa utalii ni chanzo muhimu cha ajira, mapato kwa mtu mmoja mmoja, Taifa na fursa za kibiashara kwa wananchi. Hivyo, kila mtalii aaliyepata huduma bora anakuwa balozi wa kuitangaza Tanzania kwa wengine, kurejea tena nchini na kuwashawishi watu wengine kutembelea vivutio vyetu.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Joseph Mwakabonga - Mkuu wa Operesheni Makao Makuu ya Traffic Tanzania aliwataka madereva hao kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, ikiwemo kuepuka matumizi ya simu za mkononi wakati wa kuendesha ili kulinda maisha ya watalii na watumiaji wengine wa barabara. Kwa kufanya hivyo huongeza imani kwa wageni na kuimarisha ushindani wa nchi yetu katika soko la utalii la kimataifa hasa kwa nchi zenye vivutio kama vyetu.

Patrick Mwaulambo ambaye ni Katibu wa Maafisa Usafirishaji (Terminal 2 JNIA) aliwashukuru kwa semina hiyo na kuahidi kuwa kinara wa ulinzi wa rasilimali hizo za Taifa, kutoa taarifa sahihi za uhifadhi, vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji kama walivyofafanuliwa na maafisa kutoka TANAPA huku akitilia mkazo kuwa daraja la kutoa taarifa zenye kuchagiza utajiri wa nchi yetu. Na vilevile kuwaelimisha watalii wanaowapakia katika vyombo vyao kuheshimu na kuthamini urithi wa asili wa Taifa  letu wanapotembelea tunu hizo.

Semina hiyo pia ilihudhuliwa na taasisi mbalimbali na kutoa mada wakiwema Maafisa kutoka Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama barabarani, Wadau wa Uhifadhi na Utalii, Wawakilisho kutoka Bodi ya Utalii nchini TTB, Makumbusho ya Taifa, Chuo cha Utalii Tanzania, Watoa huduma wa Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere na Kampuni ya Utalii Mtembezi.












Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI