Shirika la Hifadhi za Taifa nchini TANAPA kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo na taasisi za uhifadhi wa mazingira wameadhimisha kumbukizi ya miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere kwa kufanya matukio anuwai ikiwemo kupanda miti ya kumbukumbu kwenye taasisi za umma ikiwemo shule na maeneo mengine tukio lililofanyika chini ya Nyumba ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam, jana Oktoba 27, 2026.
Akiongoza zoezi hilo mtoto wa Baba wa Taifa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Makongoro Nyerere alisema, “Taifa litamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa uzalendo wake na moyo usio na mawaa aliokuwa nao katika kulitumikia Taifa sambamba na kupanda mbegu ya mshikamano ambayo imeendelea kuwa nguzo ya umoja na amani tunayoifurahia leo.”
Mhe. Makongoro aliwataka vijana wa Kitanzania kuwa wazalendo katika masuala muhimu na yenye maslahi kwa Taifa pia, aliwasisitiza kumuenzi Mwl. Nyerere kwa kutilia mkazo masuala ya uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na yenye vyanzo vya maji na kupanda miti kwenye makazi yao kwa ajili ya vivuli na matunda.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha Emmanuel Moirana alisema TANAPA wataendelea kuenzi mchango wa Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere kama mwanzilishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na maono yake ndio yamekuwa dira ya uhifadhi endelevu ambao matunda yake tunayashuhudia katika utalii na ongezeko la watalii nchini.
Sambamba na hilo, Kamishina Moirana aliongeza kuwa mambo mengine atayokumbukwa nayo ni pamoja na kusisitiza amani, uzalendo, mshakamano na kuwaunganisha watanzania bila kujali tofauti zao huku akiwakumbusha kuwa rasilimali za Taifa zinajukumu la kuwanufaisha watanzania wote.














0 Comments