Header Ads Widget

SIRRO ATOA MAAGIZO WAKUU WAPYA WA WILAYA KIGOMA

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MKUU wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro amewaapisha wakuu wapya wa wilaya za mkoa Kigoma walioteuliwa hivi karibuni na Rais Samia na kuwapa maagizo ya kushughulikia migogoro ya ardhi na suala la wahamiaji haramu ambalo limeleta changamoto kubwa mkoani humo.

Katika hafla ya uapisho iliyofanyika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma Mnarani mjini Kigoma Balozi Sirro alisema kuwa mkoa Kigoma umekuwa na idadi kubwa ya wahamiaji kutoka nchi za ukanda wa maziwa makuu hivyo mkoa umekuwa na idadi kubwa ya wageni ambao wanaishi bila kufuata taratibu jambo ambalo ni hatari kwa ulinzi na usalama wa nchi.

Sambamba na hilo alisema kuwa  kutokana na idadi kubwa ya wahamiaji haramu mkoa umechukua hatua madhubuti katika kutoa vitambulisho vya Taifa (NIDA) hivyo kumekuwa na malalamiko makubwa ya wananchi kunyimwa vitambulisho hivyo na kutokana na hilo amewataka wakuu hao wa wilaya kusikliliza na kufanyia kazi kwa makini jambo hilo.

“Mmechaguliwa kuja kuwatumikia wananchi hivyo msisitizo uwe kwenye kuwatumikia wananchi badala ya kuingia kwenye mgogoro wa kugombea madaraka na viongozi wenzenu, tembeleeni miradi na chukueni hatua kwa miradi ambayo mnaona ina changamoto,” Alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Awali akitoa salama za chama  Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma ,Jamal Tamim aliwakaribisha wakuu hao wa wilaya mkoani Kigoma huku akiwataka kusimamia masuala ya ulinzi na usalama ili kuufanya mkoa kuwa salama wakati wote kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo kwa uhuru.

Akizungumza baada ya uapisho huo Mkuu wa wilaya Uvinza,Mtella Mwampamba ameshukuru Rais Samia kwa nafasi hiyo na kwamba yupo tayari kutumika kwa kadri maelekezo yatakavyotolewa na kwamba amepokea maelekezo ya Mkuu wa mkoa Kigoma na yuko tayari kushirikiana na watu mbalimbali na mamlaka mbalimbali katika utekelezaji wake.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI