Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKOA Kigoma umetangaza kuwa tayari kukabiliana na maafa ya mafuriko yatakayosababishwa na mvua za El Nino kwa kuchukua hatua za tahadhari na kujiweka tayari kukabiliana na hali yeyote hatarishi itakayotokea.
Katibu Tawala wa mkoa Kigoma,Hassan Rugwa ambaye ni Katibu wa Kamati ya Maafa mkoa Kigoma alisema hayo akiwasilisha taarifa kwa Wajumbe wa kamati ya Taifa ya Maafa kuhusu utayari wa mkoa Kigoma katika kuchukua hatua za kudhibiti na kujikinga na maafa hayo.
Rugwa alisema kuwa zipo hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa ikiwemo kutoa mafunzo kwa timu mbalimbali za uratibu wa maafa zitakazoshiriki kwenye maafa hayo, kutoa elimu kwa wananchi kuchukua tahadhari, kuimarisha mifumo ya utoaji na upokeaji wa taarifa, kutambua maeneo hatarishi sambamba na kutenga maeneo ambayo wahanga watapata hifadhi kwa muda.
Awali Mratibu wa maafa ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma,Bayaga Lucas alisema kuwa makisio ya kiasi cha shilingi Bilioni 3.4 yanatarajia kutumika kwa ajili ya kugharamia mambo mbalimbali yatakayojitokeza ambapo bajeti hiyo imewasilishwa kutoka halmashauri nane za mkoa Kigoma.
Akizungumza katika kikao kazi hicho Mkurugenzi Msaidizi ofisi ya Waziri Mkuu sera,uratibu, bunge na watu wenye ulemavu, Lina Kitosi alisema kuwa kuchukua tahadhari na kuwa tayari kukabiliana na maafa ni jambo muhimu katika kuzuia madhara makubwa yanayoweza kutokea.
Kitosi alisema kuwa kuchukua tahadhari mapema kukabiliana na majanga kunaweza kusaidia kupunguza gharama ya kurekebisha uharibifu uliotokea na hivyo madhara kwa jamii na miundo mbinu mbalimbali ya utoaji huduma yanaweza kuwa na athari ndogo.
Mwisho.








0 Comments