Header Ads Widget

SERENGETI KUWA KITOVU CHA UTALII WA MICHEZO AFRIKA, UZINDUZI WA UWANJA WA GOFU FORT IKOMA WAFUNGUA FURSA MPYA ZA KIUCHUMI


Na. Edmund Salaho - FORT IKOMA, SERENGETI


Serikali ya Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuimarisha utalii wa michezo nchini kupitia uzinduzi rasmi wa Uwanja wa Golf wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, uliopo Fort Ikoma, Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, ikiwa na lengo la kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la utalii wa kimataifa, kuongeza mapato ya Taifa na kutengeneza fursa mpya za ajira.

Uzinduzi huo umefanyika leo, tarehe 18,Oktoba 2026 ukiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kubuni na kuendeleza mazao mapya ya utalii yanayounganisha uhifadhi wa maliasili, michezo na burudani.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Maliasili na Utalii  Mhe. Dkt.Ashatu Kijaji (Mb) amesisitiza kuwa uwekezaji wa uwanja huo ni hatua muhimu katika kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa michezo barani Afrika, sambamba na kuimarisha nafasi yake kama kivutio maarufu cha utalii wa wanyamapori.

Amesema utalii wa michezo, maarufu kama "Sports tourism", unaendelea kukua duniani na kutoa fursa kubwa za kiuchumi, hivyo Tanzania inapaswa kutumia fursa hiyo kuvutia watalii wa kimataifa, kuandaa mashindano ya michezo na kuongeza uwekezaji katika hoteli, usafiri, huduma za malazi na biashara nyingine zinazohusiana na utalii.





“ Uwekezaji huu unatarajiwa kuongeza mapato yatokanayo na utalii, kuvutia watalii wa kiwango cha juu, kuongeza muda wa watalii kukaa nchini, kuchochea uwekezaji na kufungua ajira mpya kwa vijana, ” amesema Dkt. Kijaji

Aidha, Kijaji ameongeza kuwa uwepo wa uwanja huo utawezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano mbalimbali ya golf katika ngazi za Afrika na kimataifa, hivyo kuongeza mwonekano wa nchi katika soko la utalii wa michezo.

Kamishna wa Uhifadhi *TANAPA,* Massana Mwishawa ameeleza kuwa usanifu wa uwanja huo umezingatia matumizi ya vikwazo vya asili, ikiwemo miti iliyohifadhiwa ndani ya eneo la uwanja, ili kuongeza upekee na changamoto kwa wachezaji.

Pia, uwanja huo haujawekewa uzio ili kuruhusu wanyamapori kuendelea kutumia eneo hilo kwa uhuru, kwa kuzingatia taratibu za uhifadhi. Mfumo wa umwagiliaji wa maji ardhini pia umewekwa kama sehemu ya hatua za kupunguza athari kwa mazingira.

Uwepo wa wanyamapori katika eneo la uwanja unatajwa kuwa miongoni mwa vivutio vya kipekee vinavyoweza kuutofautisha na viwanja vingine vya golf duniani.

“ Uwanja huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati iliyotekelezwa kwa lengo la kuboresha bidhaa za utalii, kuongeza thamani ya vivutio vya nchi na kupanua wigo wa shughuli za kiuchumi zinazotokana na uhifadhi ikiwemo wananchi wanaoishi katika maeneo jirani na Hifadhi ya Taifa Serengeti kunufaika na fursa zinazoweza kujitokeza kupitia ajira, biashara na huduma mbalimbali zinazohusiana na ongezeko la watalii ”

Uzinduzi wa Uwanja wa Golf wa Hifadhi ya Taifa Serengeti ni hatua mpya katika kuunganisha uhifadhi, utalii na michezo, huku ukifungua fursa za uwekezaji na kuimarisha ushindani wa nchi katika soko la utalii wa kimataifa.












Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI