Header Ads Widget

MVUA ZINAKARIBIA: MOROGORO YATAKIWA KULINDA MAJI SAFI


Na Matukio Daima Media, Morogoro

MAMLAKA za maji mkoani Morogoro zimetakiwa kuanza mara moja kutambua maeneo ambayo yanaweza kuathiriwa na mvua na kusababisha maji safi kuchanganyika na maji taka.

Aidha Serikali imetaka hatua za kinga zichukuliwe kabla ya changamoto zitakazosababishwa na Mvua kubwa zaidi ya wastani zinazotarajiwa kujitokeza.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amesema wataalamu wanapaswa kufanya tathmini ya haraka ya miundombinu na maeneo hatarishi, ikiwemo yale yenye uwezekano wa kukumbwa na mmomonyoko wa udongo.

Mathew ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake mkoani Morogoro, ambapo amekagua maendeleo ya mradi wa kuongeza kimo cha tuta la Bwawa la Mindu.

Amesema ukaguzi huo unapaswa kuangalia maeneo yote yanayoweza kuathiri usalama wa maji na afya za wananchi wakati wa msimu wa mvua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasy, amesema bodi hiyo ina mipango ya kuendelea kulinda vyanzo vya maji na miundombinu yake ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.

Naye mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema maandalizi ya mapema ni muhimu akisisitiza ushirikiano katika kuhakikisha maeneo yanayoweza kupata athari yanachukuliwa hatua kwa wakati.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha ulinzi wa miundombinu na kuhakikisha mvua haziathiri upatikanaji wa maji salama pamoja na afya za wananchi.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI