Na Matukio Daima Media, Morogoro
Mkoa wa Mrogoro unatarajiwa kupata uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 65 katika ujenzi wa hoteli ya nyota nne na kituo cha kisasa cha mikutano, mradi unaolenga kutumia ongezeko la wasafiri wa SGR kufungua fursa mpya za biashara, ajira na utalii.
Mradi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Shirika la Reli Tanzania (TRC) katika eneo la Stesheni ya SGR ya Jakaya Kikwete, Kihonda, unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili na nusu.
Kwa mujibu wa TRC, uwekezaji huo utakuwa na hoteli ya nyota nne yenye vyumba takribani 91 pamoja na kumbi 26 za mikutano zenye uwezo wa kuhudumia watu kuanzia 10 hadi 600 kulingana na mahitaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Clement Sangu, amesema thamani ya mradi huo haitakiwi kuishia kwenye majengo, bali unatakiwa kuzalisha ajira, biashara na mapato kwa wananchi.
Sangu amesema WCF na TRC zinapaswa kuweka ratiba ya utekelezaji, mgawanyo wa majukumu na mifumo ya ufuatiliaji ili makubaliano hayo yaende kutoka kwenye kusaini hadi utekelezaji wa mradi wenye manufaa kwa wananchi.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, akizungumza kwenye hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano wa utekelezaji mradi huo, amesema ongezeko la matumizi ya SGR limeongeza mahitaji ya malazi, mikutano, chakula, biashara na utalii katika miji inayohudumiwa na reli hiyo.
Kihenzile amesema SGR imesafirisha takribani abiria milioni 5.5 kati ya Juni 2024 na Machi 2026, huku TRC ikikusanya zaidi ya Sh bilioni 169, hali inayotoa msingi wa kuangalia mapato mengine yanayoweza kuzalishwa na mali za reli.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC, Jaffer Machano, amesema mradi huo umefika wakati muafaka kutokana na idadi ya wananchi wanaotumia SGR, akieleza kuwa wastani wa abiria wanaosafiri kati ya Dar es Salaam na Morogoro kwa siku unafikia zaidi ya 2,800.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya WCF, Renatha Rugarabamu, amesema uwekezaji huo unalenga kuimarisha uwezo wa Mfuko kuwa na vyanzo endelevu vya mapato ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mradi huo pia unatarajiwa kuongeza uwezo wa Morogoro kuwa mwenyeji wa mikutano ya kitaifa na kimataifa, huku ukifungua soko kwa hoteli, usafiri, chakula, biashara, huduma za kitaalamu na shughuli za utalii
.













0 Comments