Header Ads Widget

MKOSOAJI WA RAIS WA RWANDA ALIYEKUWA UHAMISHONI APATIKANA AKIWA AMEKATWA KICHWA

Aliyekuwa Sajenti Meja wa Jeshi la Rwanda, ambaye baadaye alijulikana kwa kuwa mkosoaji wa wazi wa Rais Paul Kagame, amepatikana akiwa amekatwa kichwa nchi jirani ya Uganda.

Robert Kabera, mwenye umri wa miaka 50, alikimbia Rwanda baada ya kushtakiwa kwa madai ya unyanyasaji wa kingono, ambayo aliyakanusha. Aliomba hifadhi nchini Uganda akidai kuwa alikuwa akifuatiliwa kwa misingi ya kisiasa.

Msemaji wa Polisi wa Uganda, Kituuma Rusoke, alisema Jumatatu kwamba kichwa cha Kabera bado hakijapatikana. Mwili wake ulipatikana na wakazi wa eneo moja lililo pembezoni mwa mji wa Kampala mwishoni mwa wiki.

Serikali ya Rwanda haijatoa tamko rasmi kuhusu mauaji hayo. Wakosoaji kadhaa wa Kagame wameuawa, ndani ya Rwanda na pia nje ya nchi.

Mjane wake, Jeanne d'Arc Rwigema Uwizeye, aliiambia BBC idhaa ya Maziwa Makuu kwa ujumbe wa maandishi kwamba sasa ana hofu kuhusu usalama wa familia yake.

“Inatisha. Nahisi kama nimechanganyikiwa. Mimi na watoto wangu hatuna usalama,” alisema.

Kwa mujibu wa familia yake, Kabera alikuwa amesafiri kwenda kukagua eneo la ujenzi lililoko takribani kilomita 45 kutoka Kampala kabla ya kuuawa.

Kabera alikuwa amejijengea umaarufu kama mwanamuziki na mtayarishaji wa maudhui kwenye YouTube. Kituo chake cha YouTube kilikuwa na zaidi ya wafuasi 144,000 na zaidi ya video 800, nyingi zikiwa zikimkosoa Kagame na utawala wake.

Likizungumzia taarifa za kuuawa kwake, kundi la upinzani lililo uhamishoni la Rwanda National Congress (RNC) lilitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina na wa uwazi ili wale wote waliohusika na mauaji hayo wafikishwe mbele ya sheria.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, RNC ilisema:

"Leo, familia yake inaomboleza, sauti yake imezimwa, na Wanyarwanda wanaoishi uhamishoni wanakabiliwa na swali la kutisha: tunaweza kuwa salama wapi?"

Kifo chake kimeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa wapinzani na wakosoaji wa serikali ya Rwanda wanaoishi uhamishoni katika mataifa mbalimbali.

Mwaka 2014, Patrick Karegeya, aliyekuwa mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi ya Rwanda na mmoja wa waanzilishi wa RNC, alipatikana amefariki katika chumba chake cha hoteli mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Tukio la kuuawa kwa Kabera limeibua tena mijadala kuhusu usalama wa wakosoaji wa serikali ya Rwanda waliopo nje ya nchi, huku mashirika ya haki za binadamu na makundi ya upinzani yakitaka uchunguzi huru ufanyike ili kubaini waliohusika na tukio hilo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI