Header Ads Widget

KILIBA AICHARUKIA CHADEMA, AHOJI UKOMAVU WAKE WA KISIASA

Na Matukio DaimaMedia

Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHILISO), Geoffrey Kilima, amehoji ukomavu wa kisiasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akisisitiza umuhimu wa vyama vya siasa kutanguliza maslahi ya taifa na kuwajibika kwa kauli na matendo yao.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kilima amesema mfumo wa vyama vingi ulioanzishwa mwaka 1992 ulilenga kujenga ushindani wa hoja na kuimarisha demokrasia, hivyo wanasiasa wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa namna inayochochea maendeleo badala ya kuongeza migawanyiko.


Amesema baada ya zaidi ya miongo mitatu ya mfumo huo, ni muhimu viongozi wa kisiasa kuonyesha ustaarabu katika mijadala, kuheshimu maoni yanayotofautiana na kuepuka lugha zinazoweza kuchochea uhasama miongoni mwa wananchi.


Kiliba pia amekosoa kile alichokieleza kuwa ni ukosefu wa mshikamano wa baadhi ya wanasiasa wakati wa misiba na majanga, akisema tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa kikwazo cha kuonyesha utu na kutoa pole kwa waliopatwa na matatizo.


Kuhusu suala la Katiba mpya, amesema mchakato huo unahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali, wakiwamo vyama vya upinzani, ili kufikia majadiliano yanayozingatia maslahi mapana ya taifa.


Amesema vyama vya siasa vinapaswa pia kujikita katika kutoa mapendekezo ya kutatua changamoto za wananchi, huku vikizingatia maendeleo katika sekta za elimu, afya, nishati na usafiri. Kwa mujibu wa Kilima, mijadala ya kisiasa inapaswa kwenda sambamba na hoja na mipango inayoweza kuboresha maisha ya wananchi.


Akizungumzia CHADEMA, Kiliba amesema chama hicho kimekuwa kikizungumzia masuala ya ufisadi, wizi wa kura na upendeleo katika ugawaji wa nafasi tangu miaka ya 2000. Hata hivyo, amehoji kama chama hicho kimeonyesha mabadiliko ya kutosha katika kushughulikia changamoto hizo ndani ya taasisi yake.


Amesema vyama vya siasa vina haki ya kutafuta ridhaa ya wananchi ili kuongoza nchi, lakini vinapaswa kueleza kwa uwazi malengo yao na kuweka mikakati ya kutatua matatizo yanayowakabili wananchi.


Kiliba amesisitiza kuwa demokrasia imara inahitaji ukweli, uwajibikaji na kuheshimu maoni tofauti, akisema viongozi wa kisiasa wana wajibu wa kulinda umoja wa taifa wanapotekeleza majukumu yao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI