Mke wa mwanadiplomasia wa Uswizi anayehudumu katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, ambaye nimzaliwa wa Uganda, ndiye mgonjwa anayepokea matibabu ya Ebola nchini Nigeria, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Uswizi imesema.
Katika taarifa yake kwa shirika la habari la Reuters, wizara hiyo imesemainaaminika kuwa mwanamke huyo aliambukizwa virusi hivyo alipokuwa akisafiri nchini Uganda.
Mumewe, ambaye aliandamana naye katika safari hiyo, pia ametengwa kwa uangalizi wa kitabibu, lakini bado hajaonyesha dalili zozote za ugonjwa huo.
Kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia magonjwa (Africa CDC) kinachunguza uwezekano wa mwanamke huyo kukutana na mgonjwa wa kwanza wa Ebola aliyethibitishwa nchini Kenya alipokuwa akisafiri kupitia Uganda mapema mwezi huu.
Inaaminika kuwa wagonjwa hao wote wawili walipitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe nchini Uganda tarehe 3 mwezi Oktoba, ingawa hadi sasa hakuna uhusiano uliothibitishwa kati yao.
Bado kuna maswali kuhusu mahali ambapo mwanamke huyo aliambukizwa virusi hivyo.
Awali, Uganda ilisema kuwa mwanamke huyo alikuwa amesafiri hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako mlipuko wa sasa wa Ebola umeenea. Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO), Africa CDC na Wizara ya Afya ya Nigeria zimesema hazijapokea taarifa zilizothibitishwa kuthibitisha safari hiyo.
Mamlaka za Nigeria zimesema awali kuwa watu 44 ambao huenda walikutana na mwanamke huyo na kuathiriwa na virusi hivyo walikuwa wametambuliwa na kuagizwa kujitenga. Hata hivyo, maafisa wa Africa CDC walisema Alhamisi kuwa watu wengine zaidi walikuwa wametambuliwa, ingawa hawakutaja idadi hiyo mpya.
Nchini Kenya, mamlaka za afya pia zimethibitisha kuwa watu wote 135 waliokutana na mgonjwa wa kwanza wa Ebola nchini humo wametambuliwa na kutengwa.
Kenya imerekodi visa tisa vya Ebola vilivyothibitishwa hadi kufikia sasa, vinavyohusishwa na msafiri aliyesafiri kutoka DRC hadi Kenya kupitia Uganda.
Waziri wa Afya wa Nigeria alisema Alhamisi kuwa mamlaka hazina ushahidi wowote unaoonyesha kuwa kisa cha Ebola kilichothibitishwa hivi karibuni nchini humo kimeenea katika jamii. Ameelezea kuwa ni kisa hicho kimoja tu ambacho kimedhibitiwa.






0 Comments