Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa Elon Musk amerejesha huduma ya mtandao wa satelaiti wa Starlink kwa Ukraine baada ya vikwazo vilivyoathiri mawasiliano ya vikosi vya Ukraine.
Kauli hiyo imekuja baada ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kusema kuwa huduma za Starshield, mtandao wa kijeshi unaotegemea mfumo wa Starlink, zilikuwa bado hazijarejeshwa kikamilifu.
Awali, Musk alikanusha madai kuwa alihusika katika kuvurugwa kwa huduma hiyo. Usumbufu huo ulitajwa kuathiri uwezo wa Ukraine kutumia ndege zisizo na rubani (droni) katika mashambulizi dhidi ya Urusi na katika kujilinda dhidi ya mashambulizi ya adui.
Alipoulizwa kuhusu taarifa kwamba alimuomba Musk kuondoa vikwazo hivyo, Trump hakuthibitisha moja kwa moja madai hayo, lakini alisema: "Jambo muhimu ni kwamba huduma hiyo imerejeshwa."
Utawala wa Trump pia umewahi kukanusha madai kwamba uliiagiza kampuni ya Musk kudhibiti huduma hiyo.
Vikwazo hivyo vya mawasiliano vilikuja wakati Trump alipokuwa akimshinikiza Zelensky kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Urusi, akidai kuwa mashambulizi hayo yalichangia kupanda kwa bei za nishati.
Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani mwezi ujao, Trump ameondoa baadhi ya vikwazo dhidi ya Urusi na kuruhusu uagizaji wa dizeli kutoka Urusi kuingia katika soko la Marekani. Hatua hiyo imekosolewa na Ukraine pamoja na washirika wake wa Ulaya.






0 Comments