Waziri wa Afya wa Nigeria, Muhammad Ali Pate, amesema mgonjwa wa kwanza kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola nchini humo amehamishiwa Uswisi kwa ajili ya matibabu.
Pate amesema hali ya mgonjwa huyo imeimarika kwa kiasi kikubwa na kwamba ana fahamu na ana uwezo wa kuwasiliana. Hata hivyo, alionya kuwa matokeo mazuri ya vipimo vya maabara hayaondoi uwezekano wa mgonjwa huyo kuendelea kuwaambukiza wengine.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, waziri huyo alisema matokeo ya vipimo vya maabara yanaonyesha maendeleo mazuri katika afya ya mgonjwa huyo.
Mgonjwa huyo alisafirishwa pamoja na mumewe, ambaye hadi sasa hajaonyesha dalili zozote za maambukizi ya ugonjwa huo.
Waziri huyo aliwapongeza wahudumu wa afya waliomhudumia mgonjwa huyo pamoja na maafisa wa afya ya umma waliosimamia zoezi la uhamisho, akisema lilifanyika kwa kuzingatia taratibu kali za afya ya umma.
Aliongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa baada ya mgonjwa huyo na mumewe kuwasili salama nchini Uswisi.
Wiki iliyopita, Nigeria ilithibitisha kisa chake cha kwanza cha Ebola katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi. Mgonjwa huyo aligundulika kuwa na aina ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo.
Wakati huohuo, mamlaka za afya nchini humo zinaendelea kuwafuatilia watu waliowasiliana na mgonjwa huyo katika juhudi za kudhibiti na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.






0 Comments