Na Matukio Daima Media
Kagera,Bukoba.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetoa mafunzo kwa maafisa na watoa huduma kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), yakilenga kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wateja na kupunguza malalamiko yanayoweza kujitokeza katika utoaji wa huduma za maji.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watumishi ili kuwahudumia wateja kwa weledi, kutumia lugha yenye staha na kuhakikisha kuwa changamoto zinazowasilishwa na wateja zinashughulikiwa kwa wakati ili kuongeza ufanisi na kuridhika kwa wananchi wanaopata huduma za maji.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Bw. Nyirabu Musira, ameeleza taratibu zinazopaswa kuzingatiwa katika kumhudumia mteja, na kusisitiza umuhimu wa kutoa huduma kwa kuzingatia weledi na kufuata utaratibu unaoweza kupunguza malalamiko kutoka kwa wateja.
Musira amesisitiza kuwa utoaji wa huduma bora unahitaji watumishi kuwa na uelewa wa mahitaji ya wateja, kuwasikiliza kwa makini na kushughulikia changamoto zao kwa njia inayozingatia taratibu na miongozo iliyowekwa na mamlaka husika.
Kwa upande wake, Afisa Huduma kwa Wateja kutoka EWURA, Bi.Jessica Sewando, amesema ni muhimu kwa wateja kusoma na kufahamu Sheria ya Maji ili waweze kuelewa haki na wajibu wao na kufuata taratibu zinazotakiwa katika kupata huduma za maji.
Aidha, Sewando amewahimiza wateja kutoa taarifa mapema wanapobaini upotevu wa maji au uharibifu wa miundombinu ya maji, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza hasara kwa mamlaka, kuepusha changamoto za upatikanaji wa maji na kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi bila ya malalamiko ya upande mmoja.
Pia Kaimu Mkurugenzi Wa Huduma kwa Mteja kutoka BUWASA,Bi Devotha Koy amewashauri EWURA kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara ili kuendelea kuwapatia uwezo na maalifa zaidi,na kuwasisitiza baadhi ya wateja kulipia bili zao kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Naye Kaimu Mkurugenzi BUWASA, Bi Julieth Shangali, ameishukuru EWURA kwa kutoa mafunzo hayo, akisema yatasaidia kuongeza uelewa kwa watumishi kuhusu namna bora ya kuwahudumia wateja na kuboresha mahusiano kati ya mamlaka hiyo na wananchi wanaotumia huduma zake.
Shangali amesisitiza kuwa BUWASA itazingatia na kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa katika mafunzo hayo, ikiwemo matumizi ya lugha yenye staha, kusikiliza wateja na kutoa huduma bora kwa wakati.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mafunzo hayo ni muhimu katika kupunguza malalamiko na kuongeza imani ya wananchi kwa mamlaka hiyo








0 Comments