Header Ads Widget

HASSAN AOMBA MSAADA BAADA YA MIEZI MINNE BILA KULA


Na Matukio Daima Media, Morogoro

Zaidi ya miezi minne bila kuweza kula, akitegemea dripu ya Maji na akiwa hana uwezo wa kujigharamia matibabu zaidi. 

Hiyo ndiyo hali inayomkabili Hassan Bryton (56), mkazi wa Mkata, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, anayehitaji msaada wa wasamaria wema ili aweze kufika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hassan amekumbwa na changamoto ya uvimbe kwenye koo unaomzuia kula, huku hali yake ikimfanya ashindwe kuendelea na shughuli iliyokuwa ikimpatia kipato ya kuchoma na kuuza mkaa.

Licha ya kuandikiwa rufaa ya kwenda Muhimbili, safari hiyo bado haijafanikiwa kutokana na ukosefu wa fedha, hali inayomlazimu kutafuta msaada wa watu wenye moyo wa kujitolea ili kupata matibabu zaidi.

Akiongea kwa tabu sana, Hassan anasema hali hiyo imebadili maisha yake kwa kiasi kikubwa, kutoka mtu aliyekuwa akijitafutia kipato hadi kutegemea msaada wa wengine katika mahitaji ya msingi.

Kwa sasa anaishi na dada yake, Amina Mohammed Malenda, mjane mkazi wa Mtaa wa Mgaza, Kata ya Mindu, Manispaa ya Morogoro, ambaye amejitwika jukumu la kumhudumia licha ya changamoto zake za maisha.

Amina ambaye ni mjane, anasema hali ya ndugu yake inahitaji msaada wa haraka, kwani uwezo wake wa kifedha ni mdogo na mahitaji ya mgonjwa yanaendelea kuwepo siku hadi siku 

Anasema hata anapokumbwa na changamoto nyingine za kiafya, familia inakabiliwa na ugumu wa kumudu gharama huku akitakiwa kwenda Muhimbili alikoandikiwa rufaa akitokea hospitali ya Jeshi ya Mzinga na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Katika kujaribu kupunguza changamoto hiyo, baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Mgaza wamekuwa wakichangishana fedha kidogo kidogo kwa ajili ya dripu na mahitaji mengine ya msingi ya familia. Hata hivyo, msaada huo haujatosha kukidhi mahitaji yote yanayomkabili Hassan.

Mmoja wa mabalozi katika Mtaa wa Mgaza, Ifrahim Kaunya, maarufu kama Teacher, anafahamu hali ya familia hiyo na juhudi zinazofanywa na wananchi katika kumsaidia mgonjwa huyo.

Hassan hana mke wala mtoto, hivyo dada yake ndiye anayemhudumia kwa sasa. Familia inaomba wadau mbalimbali, taasisi na wananchi wenye uwezo kujitokeza kumsaidia ili aweze kufika Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Kwa yeyote atakayeguswa na hali yake, msaada unaweza kufikishwa kupitia dada yake, Amina Mohammed Malenda, kwa namba ya Airtel 0684037960. Mchango wowote unaotolewa kwa nia njema unaweza kuwa hatua muhimu katika kumsaidia Hassan kupata huduma za afya anazohitaji.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI