Na Angel Magesa, Matukio Daima Media, UoI
IRINGA: Waandishi wa habari wanawake mkoani Iringa wameandaa tukio maalumu la “Wauguzi Gala – Usiku wa Heshima kwa Wauguzi” litakalofanyika Oktoba 25, 2026 katika Ukumbi wa Royal Palm, Gangilonga mkoani humo, kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa wauguzi katika utoaji wa huduma za afya nchini.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Tukuswigwa Mwaisumbe, amesema waandishi wa habari wanawake wameamua kuwaandalia wauguzi usiku huo kutokana na nafasi kubwa wanayoitoa katika kuwahudumia wananchi, hususan wagonjwa wanaofika katika hospitali na vituo mbalimbali vya afya.
Mwaisumbwe amesema wauguzi wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali za kikazi, ikiwemo msongo wa mawazo unaotokana na majukumu makubwa ya kuwahudumia wagonjwa, hivyo tukio hilo litatoa nafasi ya kupumzika, kuburudika, kushirikiana na kusikiliza simulizi za mafanikio kutoka kwa wauguzi hao.
“Tunataka kupata nafasi ya kukaa pamoja na wauguzi, kupumzika nao, kucheza na kuzungumza nao, lakini pia kusikiliza simulizi za mafanikio katika kazi wanazozifanya,” amesema Maisumbe.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Maandalizi, Leila Kazimoto, amesema tukio hilo litakuwa na utoaji wa tuzo kwa wauguzi watakaopendekezwa na chama chao, huku kukiwa na burudani, vichekesho na maonesho ya simulizi za mafanikio ya wauguzi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kazimoto amesema tiketi za kushiriki katika tukio hilo zinapatikana katika vituo mbalimbali ndani na nje ya Manispaa ya Iringa, huku akiwataka wananchi na wadau wenye nia njema kujitokeza kununua tiketi na kushiriki katika usiku huo wenye kaulimbiu “Wauguzi Wauguzi Wetu, Tunao na Tunatamba Nao.”
Naye Mhazini wa Kamati ya Maandalizi, Getrude Madembwe, amewataka kampuni, taasisi na wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini tukio hilo ili kufanikisha maandalizi yake na kuhakikisha wauguzi wanapata heshima wanayostahili kutokana na mchango wao katika jamii.
“Tumeandaa tukio hili kwa kutambua mchango wao mkubwa katika jamii, na kupitia kaulimbiu yetu ya ‘Wauguzi Wauguzi Wetu, Tunao na Tunatamba Nao tunataka kuwaonesha kuwa tunathamini kazi yao na tunajivunia kuwa nao,” amesema Kazimoto.
Madembwe amesema tukio hilo linatarajiwa kuwa la kipekee na la kwanza kufanyika kwa namna hiyo mkoani Iringa, hivyo wananchi, taasisi na wadau mbalimbali wanaombwa kushiriki na kulipa nguvu ili liweze kufanyika kwa mafanikio makubwa.
“Tunawaomba wadau wote, kampuni, taasisi na wananchi kwa ujumla kujitokeza kutuunga mkono katika tukio hili. Hii ni nafasi ya pamoja ya kuwapongeza na kuwapa heshima wauguzi kwa kazi kubwa wanayoifanya kila siku. Tushirikiane kuhakikisha Wauguzi Gala inakuwa tukio lenye mafanikio na la kukumbukwa katika Mkoa wa Iringa,” amesema Madembwe.






0 Comments