Mji wa Bagamoyo unatarajiwa kulipuka kwa burudani wakati Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo litakalofanyika Oktoba 28 hadi 31 2026, likiwakutanisha wasanii na vikundi 146 kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Septemba 2, 2026, Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Bw. Gabriel B. Kiiza, amesema kati ya vikundi hivyo, 104 vinatoka ndani ya Tanzania huku 42 vikiwa vya kimataifa.
Amesema shughuli za Tamasha zitaanza rasmi kwa mkesha utakaofanyika Oktoba 27, kabla ya kuendelea na matukio mbalimbali ya sanaa na utamaduni katika siku nne ambazo Tamasha hilo litatimua vumbi.
Katika kipindi hicho, wananchi na wageni watapata fursa ya kushuhudia burudani na maonesho mbalimbali yatakayohusisha muziki, ngoma, maigizo, sarakasi, ushairi, vichekesho, mazingaombwe na filamu.
Mbali na burudani, tamasha hilo pia litakuwa jukwaa la kukuza na kuonesha kazi za sanaa za ufundi pamoja na shughuli za biashara zinazohusiana na sanaa na utamaduni.
Kwa upande mwingine, washiriki wa tamasha watapata fursa ya kuifahamu zaidi historia na utamaduni wa Mji wa Bagamoyo kupitia ziara katika baadhi ya vivutio muhimu vya kihistoria na kiutamaduni, ikiwemo Mji Mkongwe wa Bagamoyo, Magofu ya Kaole (Kaole Ruins) na Boma la Wajerumani.
Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ni sehemu muhimu ya kuendeleza, kuhifadhi na kutangaza sanaa na utamaduni wa Tanzania, huku likitoa nafasi kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi kukutana, kubadilishana uzoefu na kuonesha vipaji vyao.









0 Comments