Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI imewataka wananchi kutumia mvua kubwa zinazotarajiwa kutokana na hali ya El-Niño kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi na uvunaji wa maji, huku ikikadiria Sh730 bilioni zitahitajika katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Niño.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema pamoja na uwezekano wa mvua hizo kusababisha mafuriko, maporomoko ya ardhi na magonjwa ya mlipuko, wananchi wanapaswa kuzitumia kama fursa ya kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha.
Amesema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri Agosti 18, 2026 kuhusu uwepo wa hali ya El-Niño yenye nguvu inayoweza kusababisha mvua kubwa na madhara mengine, hivyo maandalizi yanahitajika ili kupunguza athari na kutumia fursa zinazotokana na mvua hizo.
“Usimamizi wa maafa ni jukumu letu sote, shiriki sasa na chukua hatua,” amesema Prof Kabudi.
Amesema Serikali imekadiria Sh730 bilioni kama rasilimali zinazohitajika kutekeleza mpango huo, kiasi ambacho kinahusisha bajeti za taasisi za Serikali na wadau mbalimbali wanaoshiriki katika shughuli za kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali baada ya madhara ya El-Niño.
Hata hivyo, amefafanua kuwa fedha hizo si kiasi chote kilichotengwa na Serikali, kwani katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga Sh10 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo katika sekta zote.
Prof. Kabudi amesema makadirio ya Sh730 bilioni yamezingatia utabiri wa El-Niño kwa mwaka 2026/2027, uchambuzi wa madhara yanayoweza kujitokeza katika sekta mbalimbali pamoja na historia ya madhara yaliyotokana na matukio ya El-Niño ya miaka ya 2023/2024, 2015/2016 na 1997/1998.
Amesema sehemu ya shughuli zitakazotekelezwa ni kukarabati na kuimarisha barabara, madaraja, reli, mitaro na miundombinu ya huduma muhimu kama afya, elimu, umeme, maji na mawasiliano katika maeneo hatarishi.
Kwa upande wa wananchi, Waziri huyo amewataka kuhakikisha mvua hizo zinatumika kikamilifu kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvunaji wa maji na uvuvi, huku wakichukua tahadhari katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko.
Amesema wakulima wanapaswa kutumia mbinu bora za kilimo, kuchagua mazao yanayofaa kwa msimu wa Vuli na kutumia mbegu bora ili kunufaika na mvua hizo, pamoja na kuweka akiba ya chakula kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Aidha, amewataka wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama, huku maeneo hatarishi yakitambuliwa mapema na wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuhamasishwa kuhama kwenda maeneo salama.
Prof. Kabudi amesema mpango huo unahusisha pia kuimarisha hifadhi ya akiba ya chakula cha taifa, kuweka vifaa vya uokoaji na misaada ya kibinadamu katika maghala ya kikanda na kutenga maeneo salama kwa ajili ya makazi ya muda endapo maafa yatatokea.
Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu Agosti 26, 2026 iliwaelekeza Wakuu wa Mikoa ambayo kwa mujibu wa utabiri inaweza kuathirika na mvua za El-Niño kuchukua hatua za maandalizi ya kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza.
Waziri huyo amewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za TMA kila siku ili kuchukua hatua kwa wakati, huku akisisitiza kuwa mvua hizo zinapaswa kuonekana kama fursa ya uzalishaji pamoja na changamoto inayohitaji maandalizi.
Mwisho






0 Comments