Header Ads Widget

UGONJWA SI FURSA YA KUJIPATIA FEDHA

NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,DODOMA

WATOA  huduma za afya nchini wametakiwa kuzingatia maadili, uadilifu na huruma katika kuwahudumia wagonjwa na kuacha kuona ugonjwa wa mtu kama fursa ya kujipatia fedha.

Rai hiyo imetolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania na Makamu wa Pili wa Mwenyekiti wa CCT, Nelson Kisare, alipokuwa mgeni rasmi katika Kongamano la 89 la Chama cha Madaktari Wakristo Tanzania (TCMA), Dodoma.


"Taaluma ya udaktari inahitaji uaminifu, utu na weledi, akisisitiza kuwa ugonjwa si fursa  bali ni changamoto inayopaswa kuhudumiwa kwa haki na huruma,"Kisare amesema .


Aidha, amewataka watoa huduma kuwa waadilifu katika matumizi ya dawa, vifaa tiba na rasilimali za hospitali, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda siri za wagonjwa.


Kwa upande wake, Rais wa TCMA, Padre Gilbert Sanga, amesema mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika kuboresha huduma za afya, ikiwamo utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

Amesema afya ya akili mahali pa kazi pia ni miongoni mwa ajenda za kongamano hilo, huku akieleza kuwa taasisi za dini zina takribani vituo 900 vya afya na hospitali 100 nchini vinavyoshiriki kutoa huduma.



Katibu Mtendaji wa TCMA, Dkt. Paulina Arkard, amesema chama hicho kiko tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha Bima ya Afya kwa Wote inatekelezwa na wananchi wanapata huduma bora.

Naye Joseph Njenga, Afisa Utawala wa Hospitali ya Mtakatifu Martin, Kilwa Kivinje, amesema vituo vya vijijini bado vinakabiliwa na uhaba wa watumishi, dawa, vifaa tiba na vifaa vya maabara.

Naye Mshiriki wa kongamano hilo, Blessing Kisanga, amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo watendaji wa hospitali za kanisa katika masuala ya afya, kiroho na uzoefu wa utoaji huduma.


Amesema baadhi ya hospitali za kanisa zinakabiliwa na changamoto ya kupata watumishi mbadala baada ya watumishi wanaolipwa na Serikali kustaafu, hivyo kuhitajika utaratibu rahisi wa kupata vibali vya ajira mpya.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI