📍Kamishna Kabange ampongeza Rais Samia, asema ushindi huo umefungua milango mipya ya utalii na uwekezaji
✍️ Na Beatus Maganja, Morogoro
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imewasili rasmi mkoani Morogoro leo, Septemba 2, 2026 ikiwa na tuzo mbili za World Travel Awards 2026 zilizotwaliwa na Hifadhi zake za Selous na Mpanga-Kipengere, siku chache baada ya kutangazwa washindi katika hafla ya tuzo hizo iliyofanyika Agosti 28, 2026, Zanzibar.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya tuzo hizo, iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya taasisi hiyo Morogoro, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mlage Y. Kabange amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuitangaza Tanzania na vivutio vyake katika soko la kimataifa, akisema jitihada hizo zimechangia nchi kufahamika zaidi duniani. Ametaja filamu za Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania kuwa miongoni mwa juhudi zilizoongeza mwonekano wa Tanzania, huku akiwapongeza pia watumishi wa TAWA, wananchi na wadau wa utalii ndani na nje ya nchi waliohamasisha na kupiga kura na kuziwezesha Hifadhi zake kushinda katika mashindano hayo.
Amesema mafanikio hayo yana uzito wa kipekee kwa kuwa yamepatikana katika mwaka wa kwanza kwa TAWA kushiriki mashindano hayo.
Kabange amesema ukubwa wa ushindi huo unaonekana zaidi kwa kuzingatia ushindani wa vivutio mbalimbali barani Afrika, akifananisha mafanikio hayo na timu inayotwaa ubingwa wa Afrika katika mchezo wa soka. “Tunaongelea mashindano ya Afrika. Kama kwenye mpira, haya ni mashindano ya CAF. Sisi tumekwenda kwenye fainali ya Afrika kwa mara ya kwanza na tumetoka na ushindi. Kwa hiyo siyo kitu kidogo,” amesema Kabange.
Amesema matokeo ya ushindi huo yameanza kujionesha baada ya wadau wa utalii kuanza kutafuta taarifa za namna ya kufika Mpanga-Kipengere mara tu baada ya tuzo kutangazwa Zanzibar. Kwa mujibu wa Kabange, kampuni moja ya ndege ya Zanzibar imeonesha utayari wa kuanzisha safari za moja kwa moja kwenda hifadhini humo mara miundombinu husika itakapokuwa tayari. Amesema kuwa mwitikio huo unaashiria fursa ya kuongeza watalii, mapato, uwekezaji na manufaa kwa jamii zinazozunguka maeneo hayo.
Kutokana na fursa hizo, Kabange amewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika miundombinu, malazi na huduma nyingine za utalii katika maeneo ya TAWA. Amesema uzoefu wa mafanikio ya Selous na Mpanga-Kipengere umeipa Mamlaka ujasiri wa kuyapeleka maeneo mengine katika ushindani wa kimataifa, huku Makuyuni Wildlife Park na Hifadhi ya Pande yakiwa miongoni mwa yaliyotajwa.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Emmanuel B. Musamba, *ndc* amesema tuzo hizo zina maana kubwa kwa kuwa ni uthibitisho wa kimataifa wa ubora wa rasilimali za utalii za Tanzania na juhudi zinazofanywa katika kuzihifadhi. “Hii ni kura ya imani kwa Tanzania, ni kura ya imani ya kimataifa kwa utajiri wa rasilimali tulizonazo Tanzania, lakini pia kwa juhudi za uhifadhi na uwezo wa maeneo yetu ya wanyamapori kutoa uzoefu wa kipekee,” amesema Musamba.
Musamba amesema ushindi huo pia ni heshima kwa watumishi wa TAWA na wale waliotangulia katika jukumu la kulinda rasilimali za wanyamapori, wakiwemo waliopoteza maisha katika utekelezaji wa jukumu hilo. Amesema mafanikio hayo yanaongeza wajibu wa Mamlaka kuhakikisha usalama wa wanyamapori, ubora wa maeneo na uendelevu wake vinaimarishwa kadri Tanzania inavyopanua nafasi yake katika soko la utalii la kimataifa.
“Tuzo hizi mbili siyo mwisho, ni mwanzo wa safari,” amesema Musamba, akisisitiza kuwa heshima iliyopatikana lazima iambatane na wajibu wa kuhakikisha ukuaji wa utalii hauathiri rasilimali zinazoubeba, bali unaimarisha uhifadhi endelevu, uchumi wa jamii na mchango wa sekta hiyo kwa Taifa.
Tuzo hizo ziliwasili Morogoro zikisindikizwa na shamrashamra zilizorindima kuanzia Kituo cha Treni ya Mwendokasi (SGR) cha Jakaya Mrisho Kikwete hadi Makao Makuu ya TAWA ambako viongozi, maafisa, Askari wa TAWA , watumishi wa taasisi mbalimbali pamoja na baadhi ya wananchi walikusanyika kuzipokea.
Selous imetwaa Africa’s Leading TouristAttraction 2026, huku Mpanga-Kipengere ikitwaa Africa’s Leading Honeymoon Destination 2026 mafanikio yaliyoiwezesha TAWA kuibuka na tuzo mbili katika ushiriki wake wa kwanza.













0 Comments