Serikali ya Kenya imekanusha taarifa kwamba Rais William Ruto ameamuru wafanyabiashara wa kigeni wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo nchini kufunga shughuli zao.
Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing’oei, amesema kauli ya Rais Ruto ilichukuliwa nje ya muktadha, akieleza kuwa ilikuwa katika mjadala kuhusu Muswada wa maudhui ya ndani ambao kwa sasa uko bungeni.
Sing’oei amesema raia wa Burundi, mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, wako huru kuishi na kufanya biashara Kenya, mradi wazingatie sheria za nchi.
Amesema:
“Tunawahakikishia wafanyabiashara na wafanyakazi wa mataifa yote kwamba, wakiwa na nyaraka zinazohitajika, zikiwemo vibali vya kazi na leseni, wanalindwa kisheria kuendesha shughuli zao nchini Kenya.”
Hata hivyo, serikali ya Kenya imesisitiza kuwa kuingia nchini bila viza, au kutohitajika kupata idhini ya kielektroniki ya kusafiri, hakumpi mgeni haki ya moja kwa moja ya kufanya biashara au kuajiriwa nchini.
Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Lee Kinyanjui, amesema baadhi ya wageni wamekuwa wakitumia vibaya hadhi zao za utalii au uwekezaji kufanya shughuli ambazo haziruhusiwi chini ya masharti ya vibali vyao.
Amesema:
“Kuingia nchini bila viza au kutohitajika kupata idhini ya kielektroniki ya kusafiri, hakumpi mtu haki ya kuajiriwa, kufanya biashara au shughuli za kibiashara nchini Kenya.”
Serikali imesema wanaotaka kufanya biashara au kuajiriwa Kenya lazima wazingatie masharti ya uhamiaji, wapate vibali vinavyohitajika na kufuata sheria zinazosimamia shughuli zao.
Aidha, wageni watakaobainika kukiuka masharti ya viza au vibali vyao wanaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kufutiwa hadhi au vibali vyao.
Wakati h uo huo, Ubalozi wa Burundi nchini Kenya umewafahamisha raia wote wa Burundi wanaotaka kurejea nchini kwao kuwa umeandaa utaratibu wa kuwapatia hati ya kusafiria ya muda, yaani laissez passer, bila malipo kuanzia leo Jumatatu.
Kauli hizi zinakuja baada ya Rais William Ruto kuzungumzia ushiriki wa wageni katika biashara ndogo nchini Kenya, suala lililozua mjadala kuhusu nafasi ya wafanyabiashara wa kigeni katika uchumi wa Kenya.






0 Comments