Header Ads Widget

PSPTB YATAJA UFAULU WA MITIHANI, 39 WAKOSA MITIHANI HUSIKA

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma


BODI ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imesema watahiniwa 275, sawa na asilimia 52.1, wamefaulu Mitihani ya Kati Awamu ya Pili ya mwaka 2026, kati ya watahiniwa 528 waliofanya mitihani hiyo.


Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, amesema hayo kupitia taarifa ya Bodi kuhusu mitihani hiyo iliyofanyika nchini kuanzia Agosti 30 hadi Septemba 4, 2026.


Amesema jumla ya watahiniwa 567 walijiandikisha kufanya mitihani hiyo, lakini watahiniwa 528 ndio waliofanya, huku 39 wakikosa kufanya mitihani kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo dharura.

Mbanyi amesema watahiniwa 232, sawa na asilimia 43.9, walirudia masomo yao, huku watahiniwa 21, sawa na asilimia 4.1, wakifeli na kuanza upya masomo yao katika ngazi husika.


" PSPTB imetoa nafasi kwa watahiniwa walio katika hadhi ya referral status kufanya mitihani katika kikao cha Novemba 2026, huku baadhi waliopewa last chance wakitakiwa kutumia fursa hiyo kufanya mitihani iliyopangwa kuanza Novemba 9 hadi 13, 2026," Amesema Mkurungenzi Mtendaji huyo.


Na Kuongeza "Dirisha la usajili kwa ajili ya mitihani hiyo lilifunguliwa Septemba 8, 2026 na litafungwa Oktoba 24, 2026," Amesema


Aidha, Mbanyi amewataka watahiniwa waliopata sifa za kutunukiwa vyeti vya Professional Diploma, Graduate Professional na CPSP kukamilisha taratibu zinazohitajika ili kupata vyeti vyao.


Ametoa wito pia kwa waandishi na wakufunzi kutoka vyuo vya mafunzo ya ununuzi na ugavi kuwaandaa watahiniwa ipasavyo ili waweze kufanya vyema katika mitihani hiyo.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI