Meli ya kivita ya Marekani yenye uwezo wa kurusha makombora, USS Ross, imewasili katika bandari ya Mombasa kwa ziara iliyopangwa, huku Marekani na Kenya zikisisitiza ushirikiano wao katika masuala ya usalama wa baharini na utulivu wa kikanda.
USS Ross, aina ya Arleigh Burke, iliwasili Mombasa Septemba 5 ikiwa katika operesheni za Jeshi la Wanamaji la Marekani katika eneo la Afrika na Ulaya.
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Kenya, Susan M. Burns, amesema ziara hiyo inaonyesha nguvu ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
“Ziara hii inaonyesha nguvu ya ushirikiano wa Marekani na Kenya na historia yetu ndefu ya kufanya kazi pamoja katika masuala ya kikanda yenye maslahi ya pamoja,” alisema.
Burns amesema bandari za kikanda kama Mombasa zinawezesha vikosi vya Marekani kupata huduma za vifaa, kuongeza mafuta na mahitaji mengine muhimu, huku ziara za meli zikisaidia pia kubadilishana uzoefu kati ya wanajeshi wa Marekani na wenzao wa Kenya.
Kamanda wa USS Ross, Cmdr. Pia Chapman, amesema ziara hiyo pia inawapa wanajeshi wa meli hiyo nafasi ya kupumzika baada ya muda wa operesheni.
“Wanajeshi wetu wamefanya kazi kwa bidii kubwa katika kipindi hiki cha operesheni, wakitekeleza majukumu yao kwa nidhamu na mshikamano,” alisema Chapman.
Ameongeza kuwa wanajeshi hao wanathamini mapokezi waliyopewa na wakazi wa Mombasa na fursa ya kushirikiana na jamii pamoja na washirika wao wa Kenya katika masuala ya baharini.
Kenya hushiriki kila mwaka katika zoezi la Cutlass Express, linaloongozwa na Marekani na kuwaleta pamoja washirika wa kimataifa katika kuimarisha usalama wa baharini Afrika Mashariki na Bahari ya HindiMarekani imesema inaendelea kushirikiana na Kenya kukabiliana na vitisho vya pamoja, vikiwemo kundi la al Shabaab na Islamic State.
USS Ross imekuwa katika eneo la operesheni la Fifth Fleet ya Marekani tangu Aprili, ambako kwa mujibu wa taarifa hiyo imekuwa ikiunga mkono Operation Epic Fury na kizuizi cha Marekani dhidi ya Iran.
Meli hiyo ilianza safari yake ya operesheni mwezi Machi ikiwa sehemu ya George H.W. Bush Carrier Strike Group, inayojumuisha meli ya kubeba ndege USS George H.W. Bush pamoja na meli nyingine za kivita.
Kwa sasa USS Ross inaendesha shughuli katika eneo la Sixth Fleet ya Marekani, inayohusika na operesheni za kijeshi na majini barani Ulaya na Afrika kwa kushirikiana na washirika na mataifa mengine.






0 Comments