Na Matukio Daima Media, Dar es salaam
Hofu iliyotanda miongoni mwa washiriki wa mkutano wa kitaifa wa kutafakari hali ya kisiasa nchini baada ya Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, kuanguka ghafla wakati akihutubia, sasa imeanza kutoweka baada ya taarifa kutoka kwa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwamba kiongozi huyo anaendelea vizuri.
Jaji Warioba alipata changamoto hiyo leo wakati akiendelea kutoa hotuba yake katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, hali iliyosababisha shughuli za mkutano kusitishwa kwa muda.
Baada ya kuanguka na kupoteza fahamu, alipewa huduma ya kwanza kabla ya kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Mwenyekiti wa TCD, Dorothy Semu, amewatoa hofu washiriki na wananchi waliokuwa wakifuatilia tukio hilo, akisema Jaji Warioba anaendelea vizuri.
Tukio hilo limetokea katika mkutano ambao TCD imewakutanisha wadau mbalimbali kujadili hali ya kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu demokrasia na mchakato wa Katiba.
Kwa sasa, taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa TCD imepunguza hofu iliyojitokeza baada ya tukio hilo, huku Watanzania wakiendelea kumtakia Jaji Warioba afya njema.
Mwisho






0 Comments